Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema ni muhimu kuwepo ujumuishi pamoja na ushirikishwaji wa sekta mbalimbali pamoja na jamii katika kukabiliana na changamoto zinazokwamisha ustawi wa watoto na wanawake.
Makamu wa Rais amesema hayo leo tarehe 1 Februari 2023 wakati akizindua Mkakati wa Kidunia kwa Kanda ya Afrika wa kutokomeza Ukimwi kwa Watoto ifikapo mwaka 2030, katika mkutano unaofanyika katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Dar es salaam. Amesema nchi zote kwa pamoja ni lazima kutambua vema jukumu lake ili kufikia lengo la kukomesha Ukimwi kwa Watoto ifikapo 2030 ikiwa ni pamoja na kushirikisha sekta binafsi katika azma hiyo muhimu.
Amesema ili kufanya Muungano huo wa kutokomeza Ukimwi kwa Watoto kuwa wa maana, halisia na wenye mafanikio ni lazima nchi za Afrika kuendelea kuchukua hatua za makusudi kuweka sera na mikakati muhimu, kujenga uwezo na kuendelea kufuatilia na kutathmini maendeleo ya hatua mbalimbali za mapambano hayo. ameongeza kwamba ni muhimu kujitolea kamili kwa nia na kusudi pamoja na kuwa na mipango ya kuwalinda watoto, wanawake na vijana dhidi ya matukio ya hatari na yasiyo ya lazima kama vile ndoa za utotoni, ukatili wa kijinsia na mila zote zinazowaweka hatarini ikiwemo ukeketaji.
Makamu wa Rais Dkt. Mpango amesema Serikali ya Tanzania imedhamiria kukomesha janga la Ukimwi kama tishio kwa afya ya jamii ifikapo mwaka 2030, ikiwa ni sehemu ya Malengo ya Maendeleo Endelevu. Amesema Kufikia Septemba 2022, asilima 92 ya watu walijua hali yao ya maambukizi huku asilimia 98.3 wakiwekwa katika mpango wa matumizi ya dawa za kupunguza makali ya Ukimwi (ARVs). Aidha amesema Serikali ya Awamu ya 6 kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Global Fund, PEPFAR na sekta binafsi inaendelea kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika maabara za VVU za utunzaji na upimaji wa kawaida ambapo katika kipindi cha miaka miwili imefanikiwa kutoka katika maabara 54 hadi Maabara 130.
Kwa upande wake Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema Muungano huo umelenga kupunguza sababu zote zinazopelekea vifo vya mama na mtoto. Ameongeza kwamba mataifa yanapaswa kujitoa kwa mipango na vitendo kufikia malengo ya kutokomeza Ukimwi kwa watoto ifikapo mwaka 2030.
Waziri Ummy ameongeza kwamba mkakati huo unaenda sambamba na Mpango wa Maendeleo wa Miaka mitano wa 2020/2021- 2025/2026 wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mpango Mkakati wa Wizara ya Afya wa mwaka 2022-2025 pamoja na Mkakati wa Wizara ya Afya wa Kukabiliana na Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.
Akihutubia Mkutano huo Makamu wa Rais ambaye pia ni Waziri wa Afya wa Zimbabwe Mheshimiwa Generali (Mstaafu) Constantino Chiwenga amesema Zimbabwe ipo tayari katika kuyatimiza na kufikia malengo yaliowekwa katika kukabiliana na tatizo la Ukimwi kwa watoto na kutokomeza ifikapo 2030. Amesema mkutano huo unapaswa kuwa chachu ya kila nchi kutimiza malengo yake na sio kuwa mazungumzo pekee.
Generali (Mstaafu) Constantino Chiwenga ameongeza kwamba uwekezaji katika afya ya watoto inapaswa kuchukuliwa kama jambo la lazima hivi sasa na sio hiari kwani ndio taifa la kesho. Ameongeza kwamba Zimbabwe itatumia mfumo wa kushirikisha jamii katika kukabiliana na maambukizi ya VVU kwa watoto ikiwemo kuzitambua changamoto za wazazi wanaoishi na maambukizi ili kudhibiti maambukizi hayo kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto. Aidha amesema Zimbabwe itaongeza Bajeti, pamoja na kuweka mfumo wa uwajibikaji katika kufuatilia maazimio yaliofikiwa ikiwemokupambana na matendo maovu kama ukatili wa kijinsia katika jamii ili kufikia lengo la kutokomeza Ukimwi kwa watoto ifikapo 2030.
Muungano wa Kimataifa wa kutokomeza Ukimwi kwa Watoto ifikapo mwaka 2030 kwa kanda ya Afrika unajumuisha nchi 12 zilizojiunga awamu ya kwanza ambazo ni Tanzania, Cameroon, Ivory Coast, Kenya, Zambia, Zimbabwe, Uganda, Nigeria, Afrika Kusini, Msumbiji, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Angola. Mawaziri wa Afya kutoka nchi wanachama wametoa kauli za utayari wao na jitihada zitakazofanyika katika kutokomeza Ukimwi kwa watoto ifikapo 2030.