Makamu wa Rais ataka ulinzi maeneo ujenzi wa miradi kuepusha migogoro ya ardhi

Jul, 10 2024

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Kigoma kulinda maeneo yaliyotengwa kwaajili ya ujenzi wa miradi ya maendeleo ili kuepusha kuvamiwa na hivyo kuepelekea migogoro baadae.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akikagua eneo la ujenzi wa Ujenzi wa Hospitali ya Kanda ya Magharibi na Ujenzi wa Kampasi ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Afya Muhimbili (MUHAS) Kanda ya Magharibi yaliyopo Manispaa ya Kigoma Ujiji wakati akiwa ziarani mkoani Kigoma. Amesema Miradi hiyo ni muhimu sana kwa maendeleo ya mkoa wa Kigoma na kanda nzima ya magharibi kwa ujumla hivyo yanapaswa kutengenezewa mpaka wa barabara ili kuepusha uvamizi.

Makamu wa Rais ameagiza Wakala ya Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) kuhakikisha inaanza ujenzi wa barabara kuelekea katika eneo hilo la mradi ili kurahisisha upelekaji wa vifaa vya ujenzi wakati wa utekelezaji wa mradi.

Aidha ametoa wito wa kuzingatia ratiba katika kuanza kutekelezwa kwa miradi hiyo ambayo imetengewa shilingi bilioni 4 kwa mwaka wa fedha 2024/2025 katika kuanza ujenzi wa Jengo la wagonjwa wa nje (OPD. Pia amemuagiza Mkuu wa Mkoa kuongeza hekari 50 zinazohitajika kama nyongeza katika mradi huo.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amekagua kupokea taarifa ya maendeleo ya ukarabati na upanuzi wa Uwanja wa Ndege Kigoma unaoendelea kutekelezwa mkoani humo.

Akizungumza na wananchi wanaofanya kazi katika mradi huo, Makamu wa Rais amesema serikali itahakikisha miradi hiyo inawanufaisha wananchi na kuwasisitiza kufanya kazi kwa bidii na uaminifu kwa manufaa ya mkoa na Taifa kwa ujumla.

Kazi ya ukarabati na upanuzi wa Uwanja huo inahusisha Ujenzi wa Jengo la Abiria, maegesho yan ndege, njia za kurukia ndege, mnara wa kuongoza ndege, taa za kuongoza ndege pamoja na barabara za kuingia na kutoka katika uwanja huo. Mradi huo unatarajiwa kukamilika Desemba 2025.

Settings