Makamu wa Rais ashiriki Mkutano wa Dharura wa SADC

Mar, 23 2024

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Ushirikiano katika Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC Organ Troika),Nchi za Msumbiji na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pamoja na Nchi zinazochangia vikosi katika jeshi la utayari la SADC lililopo nchini Msumbiji (SAMIM) na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (SAMIDRC) unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Mulungushi kilichopo Lusaka nchini Zambia.

Akifungua Mkutano huo Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa SADC ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Hakainde Hichilema ametoa wito kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) kutambua jukumu la kufanya kazi kwa pamoja ili kumaliza changamoto za kiusalama zinazozikabili Jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji na Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Rais Hichilema amesema kutoimarika kwa hali ya usalama na amani katika maeneo hayo kunaathiri Jumuiya katika kufikia maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kuwa rasilimali zinatumika kurejesha amani katika maeneo hayo. Ametoa wito wa kuendelea kuunganisha nguvu pamoja ikiwemo kushirikisha jumuiya za kimataifa rafiki kama vile Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.

Mkutano huo umehudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Hakainde Hichilema, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Mhe. Felix Tshisekedi, Rais wa Zimbawe Mhe. Emmerson Mnangagwa, Rais wa Malawi Mhe. Dkt. Lazarus Chakwera, Rais wa Angola Mhe. João Lourenço, Rais wa Jamhuri ya Msumbiji Mhe. Filipe Nyusi, Makamu wa Rais wa Namibia Mhe. Netumbo Nandi-Ndaitwah, Waziri Mkuu wa Lesotho Sam Matekane.

Settings