Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Tume ya Mipango wakiongozwa na Katibu Mtendaji wa Tume hiyo Bw. Lawrence Mafuru,mazungumzo yaliyofanyika Jijini Dodoma tarehe 05 Februari 2024.
Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais ametoa wito kwa wataalamu wa mipango ikiwemo idara kuu ya takwimu nchini kutambua dhamana kubwa waliyopewa katika kuandaa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Amesema Dira bora zaidi ya maendeleo ni lazima iandaliwe katika taarifa na takwimu sahihi hivyo amewataka wataalamu kuhakikisha wanaandaa takwimu halisi za maendeleo.
Makamu wa Rais ameiasa Tume ya Mipango kuzingatia makundi yote muhimu katika jamii wakati wa uandaaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ili kupata maoni yaona baadae dira hiyo kuweza kukidhi mahitaji ya wananchi. Amesema katika uandaaji wa Dira ya Maendeleo ni muhimu kuwekeza akili na ubunifu na kuzingatia malengo makubwa yatakayoweza kufikiwa.
Pia, Makamu wa Raisnamezitaka sekta mbalimbali zitakazoshiriki katika kuandaa Dira hiyo kutambua wajibu wa kutoa takwimu sahihi zinazohusiana na sekta zao.
Halikadhalika, Makamu wa Rais ametoa rai kwa sekta binafsi kuwa mstari wa mbele katika kutoa takwimu na maoni yanayohusiana na sekta zao ambazo zitaweza kuharakisha maendeleo ya nchi.
Pia Makamu wa Rais ametoa wito kwa watanzania kujitokeza katika kutoa maoni wakati wa uandaaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Amesisitiza umuhimu wa vijana kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi kutoa maoni yao kwa kuzingatia idadi kubwa ya watanzania ni vijana.