Makamu wa Rais akagua mradi wa kutibu majitaka Arusha

Mar, 14 2022

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ametembelea na kukagua mradi wa kuondoa majitaka katika jiji la Arusha uliopo eneo la Maskilia mkoani Arusha. Mradi huo una uwezo wa kutibu majitaka lita milioni 22 kwa siku ukiwa ni sehemu ya mradi mkubwa wa maji wa bilioni 520 unaotarajiwa kuwapatia maji safi na salama wakazi wamkoa wa Arusha.

Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo, Makamu wa Rais ameitaka wizara ya maji kwa kutumia mradi huo wa majitaka kwaajili ya kilimo cha umwagiliaji ili kuwasaidia wananchi wa eneo la Maskilia na maeneo jirani. Ameitaka wizara kutafuta teknolojia rafiki kupitia shirika la kimataifa la mazingira (UNEP) itakayowezesha uchakataji wa maji hayo kwaajili ya kilimo. Amesema mradi huo utaongeza ajira pamoja na kuongeza uzalishaji katika kilimo.

Makamu wa Rais amezungumza na wananchi wa mtaa waMaskilia ambao wamemueleza changamoto ikiwemo ukosefu wa majisafi na salama pamoja na changamoto ya umeme na barabara. Makamu wa Rais ameigiza wizara ya maji kushughulikia haraka changamoto ya maji safi katika eneo hilo.

Akiwa njiani Makamu wa Rais amewasalimia wanafunzi wa shule ya sekondari Mkonoo ambao walimueleza changamoto za kukosekana kwa walimu wa masomo ya sayansi wa kutosha pamoja na kutokuwepo na bweni ili kusaidia huduma ya malazi kwa wanafunzi hao.

Makamu wa Rais amesema serikali itashughulikia changamoto hizo na kuwataka kusoma kwa bidii katika wakati huu ambao serikali inagharamia elimu na wao kusoma bila ada pamoja na kuboresha miundombinu ikiwemo madarasa na madawati.

Aidha Makamu wa Rais amewasalimu wananchi wa Mkonoo na kuwataka kuendelea kuweka mazingira safi ikiwemo kupanda miti. Aidha amewahimiza kushiriki katika sensa ya watu na makazi itakayofanyika mwaka huu na kusema kwamba sensa hiyo itasaidia kufahamu idadi halisi ya watu pamoja na kusaidia namna ya kupanga mipango ya maendeleo.

Makamu wa Rais ameiagiza wizara ya maji kwa kushirikiana na viongozi ya jiji la Dodoma kuanza mchakato wa mradi wa kutoa majitaka utakaoweza kusaidia katika kilimo cha umwagiliaji katika jiji la Dodoma kwa kujifunza kupitia mradi uliopo Arusha.

Kwa upande wake Waziri wa Maji Jumaa Aweso amesema changamoto za maji katika jiji la Arusha zinaendelea kutatulia ambapo mwezi juni mwaka 2022 mradi mkubwa wa bilioni 520 utakua umekamilika na kumaliza changamoto hiyo.

Settings