Makamu wa Rais aipa kibarua Wizara ya Afya

Feb, 10 2024

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ameielekeza Wizara ya Afya kuhakikisha Kituo cha Afya Ketumbeine kilichopo Wilaya ya Longido kinapata gari la kubeba wagonjwa kutokana na changamoto za usafiri zilizopo katika Wilaya hiyo.

Makamu wa Rais amesema hayo wa uzinduzi wa Kituo cha Afya Ketumbeine kilichopo Kijiji cha Armanie Wilaya ya Longido akiwa ziarani mkoani Arusha Februari 10, 2024.

Aidha amemuelekeza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi kuhakikisha kituo hicho cha afya kinapata vifaa tiba pamoja na watumishi wa afya wanaokidhi mahitaji ndani ya muda mfupi kadri inavyowezekana.

Halikadhalika Makamu wa Rais amemuelekeza Mtendaji Mkuu wa TANROAD kukamilisha upembuzi yakinifu wa barabara ya Longido – Oldonyo Lengai (KM 98) haraka iwezekanavyo ili iweze kujengwa kwa kiwango cha lami.

Aidha ameitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuipa kipaumbele Wilaya ya Longido ambayo wakazi wake ni wafugaji kwa kuongeza mabwawa ya kunyweshea mifugo na kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kulinda malisho.

Makamu wa Rais amewataka wananchi wa Longido kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu kwa kufuata miongozo inayotolewa na Wataalam wa Afya akiwasisitiza kuzingatia usafi wa mazingira na mwili ili kujiepusha na magonjwa yanayoweza kuzuilika.

Pia Makamu wa Rais ameutaka uongozi wa Mkoa wa Arusha na Wilaya ya Longido kuhakikisha wanachukua hatua kwa yeyote atakayebainika kuhusika na vitendo vya uharibifu wa mazingira. Amesema wapo wananchi wanaoharibu mazingira kwa kufanya shughuli za ufugaji na kutafuta malisho ya wanyama kiholela ikiwamo kuchoma moto hovyo katia wilaya hiyo hali inayosababisha changamoto kubwa ya mabadiliko ya tabianchi yanayopelekea kutotabirika kwa misimu ya mvua pamoja na kusababisha ukame.

Makamu wa Rais amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua Sekta ya afya inagusa maisha ya watanzania na ustawi wa Taifa kwa ujumla na katika dhamira hiyo, Serikali imeendelea kutekeleza mikakati ya kuimarisha huduma za afya nchini ili kufikia lengo la wanachi wote kufikiwa na huduma za afya ifikapo mwaka 2030. Ujenzi wa Kituo cha Afya Ketumbeine umegharimu shilingi bilioni 1.3.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amezindua Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza katika Kijiji cha Armanie Wilaya ya Longido mkoani Arusha.

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy amesema jumla ya vijiji 11720 sawa na asilimia 95, vimeshapata huduma ya umeme na vijiji 598 vilivyosalia vitafikiwa na huduma hiyo ifikapo mwezi Juni 2024.

Settings