Makamu wa Rais ahimiza utunzaji mazingira kulinda ikolojia

Oct, 16 2025

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema suala la utunzaji wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi linapaswa kupewa kipaumbele katika uendelezaji na ukuzaji utalii ili kuepukana na kuvurugika kwa ikolojia na hatari dhidi ya ustawi wa shughuli za utalii.

Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akizindua Jengo la Makumbusho ya Eneo la Hifadhi ya Urithi wa Kijiolojia la Ngorongoro – Lengai lililopo Karatu mkoani Arusha. Amesema kutokana na uharibifu wa mazingira, inashuhudiwa muingiliano kati ya wanyamapori na binadamu unaopelekea athari kubwa zaidi, vikiwemo vifo na uharibifu wa makazi na mazao.

Aidha, Makamu wa Rais ametoa rai kwa Wizara ya Maliasili na Utalii, kupitia Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kuhakikisha miundombinu ya makumbusho hayo inatunzwa na kutumika kama ilivyokusudiwa. Vilevile, amesema ni muhimu kuweka utaratibu mzuri utakaowezesha ukarabati na matengenezo ya mara kwa mara ya miundombinu na mifumo iliyowekwa katika jengo hilo.

Halikadhalika , Makamu wa Rais ameitaka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kufanya jitihada za makusudi kushirikisha jamii inayozunguka eneo hilo katika shughuli za uhifadhi wa eneo hilo, zikiwemo mila na tamaduni zake. Pia ametoa wito kwa Watanzania, kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio na maeneo ya kihistoria ili kujifunza na kujionea utajiri mkubwa ambao nchi imejaaliwa.

Makamu wa Rais amesema ni vema Wizara kwa kushirikiana na Taasisi zake ikiwemo Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, ihakikishe inatoa mafunzo stahiki kwa watumishi watakaohudumu katika eneo hilo ili kuwawezesha watumishi hao kutumia mifumo iliyopo na kutoa huduma kwa ufasaha na ufanisi. Amesema kwa kadri itakavyowezekana, mafunzo hayo yashirikishe wadau wa utalii ambao wana mchango katika kuleta wageni watakaokuja kujifunza kupitia utalii wa mambo mbalimbali yaliyopo katika kituo hicho.

Makamu wa Rais amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali za makusudi ili kuhakikisha inaboresha huduma za utalii, ikiwemo kutengeneza filamu mbili maarufu za Tanzania: The Royal Tour” na Amazing Tanzania” . Hatua nyingine zilizochukuliwa ni pamoja na kuboresha miundombinu mbalimbali ya utalii hususan barabara, hoteli, nyumba za kulala wageni, viwanja vya ndege na nyinginezo. Pia, kurahisisha upatikanaji wa visa, kuimarisha usalama wa watalii, kuwekeza katika maendeleo ya rasilimaliwatu na kuimarisha taswira ya Tanzania duniani.

Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana amesema mageuzi makubwa yaliyofanyika katika Wizara hiyo yamepelekea kuimarika kwa sekta ya utalii kwa kuongeza watalii wa kimataifa kutoka watalii milioni 1.8 mwaka 2023 hadi kufikia watalii milioni 2.1 mwaka 2024. Pia amesema idadi ya watalii wa ndani kuongezeka kutoka milioni 1.9 hadi milioni 3.2.

Halikadhalika ametaja mafanikio mengine ni pamoja na kuimarika kwa ulinzi na usimamizi wa wanyamapori kupitia mkakati madhubuti wa kudhibiti ujangili, kuimarisha doria na matumizi ya teknolojia. Amesema idadi ya wanyamapori inazidi kuongezeka pamoja na hali ya usalama katika maeneo ya hifadhi.

Mradi wa Jengo la Makumbusho ya Eneo la Hifadhi ya Urithi wa Kijiolojia la Ngorongoro – Lengai umegharimu shilingi bilioni 32 na kufadhiliwa na Serikali ya China.

Settings