Makamu wa Rais ahimiza upendo nyakati za changamoto

Jun, 23 2023

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amewahimiza wananchi kutobaguana kwa itikadi za kisiasa wakati wa changamoto mbalimbali ikiwemo msiba unapotokea katika jamii.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akiwafariji wafiwa na waombolezaji waliojitokeza katika Ibada ya kuaga mwili wa marehemu Midlaster Daniel Nsanzugwako ambaye ni Mke wa aliyekuwa Mbunge wa Kasulu Mjini Ndugu. Daniel Nsanzugwako iliofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Usharika wa Bethel – Kasulu mkoani Kigoma leo tarehe 23 Juni 2023.

Amesema ni muhimu kushikamana vema wakati changamoto zinapojitokeza lakini pia kuendelea kutenga muda kwaajili ya kumuomba Mungu wakati wote wa Maisha hapa duniani licha ya majukumu na kazi zilizopo. Aidha Makamu wa Rais amewaasa wananchi hao kujifunza kutumikia wengine katika jamii kama ilivyokuwa kwa marehemu Midlaster Nsanzugwako.

Ibada hiyo imehudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Joyce Ndalichako, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye, Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kigoma Jamal Tamim, Viongozi wa Dini na Serikali pamoja na wananchi wa mbalimbali.

Settings