Makamu wa Rais achagiza makampuni uwekezaji wa viwanda

Jul, 31 2023

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa makampuni pamoja na viwanda hapa nchini kuwekeza zaidi katika kuongeza uzalishaji wa vifungashio ili kusaidia upatikanaji wake kirahisi na kupunguza gharama wanazopata wajasiriamali kuagiza nje ya nchi.

Makamu wa Rais ametoa wito huo leo tarehe 31 Julai 2023 wakati wa hafla ya uzinduzi wa Kiwanda cha kusindika Mboga mboga, Matunda na Viungo (Mbeya Food Park) kilichopo kata ya Iyela Jijini Mbeya. Pia ameiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha kutafuta namna ya kuweka kodi rafiki katika uzalishaji wa vifungashio ili kuwezesha upatikanaji wa bidhaa hiyo nchini.

Aidha ametoa rai kwa taasisi za fedha ikiwemo mabenki kubuni huduma rafiki na madirisha mahususi yatakayowezesha wajasiriamali kukopa kwa riba nafuu ili kuendeleza biashara zao.

Makamu wa Rais amesema Serikali ya Awamu ya Sita kwa kushirikiana na wadau wa kilimo itaendelea kutatua changamoto zilizopo katika sekta hiyo ili kuwafanya wakulima na wajasiriamali kuweza kunufaika na kilimo hapa nchini. Amewataka wakulima kuongeza uzalishaji wa mboga mboga na matunda ili kukiwezesha kiwanda hicho kufanya kazi kwa uwezo wake kamili pamoja na kukidhi mahitaji ya bidhaa hizo katika masoko mbalimbali duniani.

Pia Makamu wa Rais ametoa wito kwa a watafiti na vyuo vya utafiti, sido na taasisi zingine kuwekeza katika kufanya utafiti ili kujua mazao mbalimbali yanayotokana na bidhaa za mboga mboga zinazozalishwa nyanda za juu kusini. Pia amewasihi wabunifu, watafiti na taasisi za teknolojia kuwekeza katika kubuni mashine za kuchakata mazao na utengenezaji wa vifungashio.

Makamu wa Rais ametoa rai kuharakishwa kwa ujenzi wa vyumba vya kuhifadhia mboga mboga na na matunda (cold room) ili kuwezesha mazao hayo kusafirishwa moja kwa moja kutokea mkoani Mbeya kwa kutumia ndege ya mizigo ilionunuliwa na serikali.

Ujenzi wa Kiwanda cha kusindika Mboga mboga, Matunda na Viungo (Mbeya Food Park) pamoja na mashine zake umegharimu shilingi bilioni 1.7 iliowezeshwa kupitia mradi wa KIBOWAVI unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) chini ya Programu ya AGRI-CONNECT.

Katika hatua nyingine , Makamu wa Rais amezindua Tawi la Chuo cha Biashara (CBE) mkoani Mbeya lililopo katika kata ya Iganzo Jijini Mbeya.

Akizungumza mara baada ya kuzindua tawi la chuo hicho, Makamu wa Rais amewataka walimu na wakufunzi wa chuo hicho kusimamia elimu inayotolewa kuhakikisha inawawezesha vijana kufanya biashara endelevu kwa vitendo mahali popote. Amesema biashara ni moja ya shughuli muhimu katika taifa lakini kwa miaka mingi inakabiliwa na ufanyaji wa mazoea.

Ametoa rai kwa wanafunzi watakaopata elimu katika chuo hicho kutumia vema nafasi hiyo kwa kutojihusisha na mambo mengine kinyume na uwekezaji unaofanyika wenye lengo la kuwasaidia kuwa wafanyabiashara mahiri katika taifa.

Settings