Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ameungana na viongozi na wananchi mbalimbali katika Ibada ya kuaga mwili wa aliyewahi kuwa Msajili wa Hazina marehemu Dkt. Oswald Mashindano iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Epifania – Mtoni Kijichi Jijini Dar es Salaam leo tarehe 30 Novemba 2024.
Akizungumza na waombolezaji mbalimbali mara baada ya Ibada ya kuaga mwili wa marehemu Dkt. Oswald Mashindano, Makamu wa Rais amesema marehemu Dkt. Mashindano alikua mchapakazi, mtu mwenye busara, mkarimu na rafiki wa wote.
Amesema marehemu Dkt. Mashindano alikua na moyo wa kujitolea ambapo aliwasaidia watu mbalimbali pindi walipokumbwa na changamoto mbalimbali.
Makamu wa Rais, amewasihi Watanzania kutimiza wajibu kwa bidii zote katika nafasi mbalimbali walizojaaliwa na Mwenyezi Mungu.
Marehemu Dkt. Oswald Mashindano ambaye aliwahi kuwa Msajili wa Hazina mwaka 2016 -2018 amefariki tarehe 27 Novemba 2024 na amezikwa leo tarehe 30 Novemba 2024 katika Makaburi ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam.