Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2024 ahamasisha upandaji wa miti

Apr, 03 2024

Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Bw. Godfrey Mnzava amesema kila wanapokwenda katika Halmashauri lazima wakute watu wameshapanda miti sababu jambo hilo sio la kushtukiza.

Bw. Mnzava amesema kumekuwa na tabia ya baadhi ya viongozi kupanda mti pale wanapoona Mbio za Mwenge unapita baada ya hapo hakuna kinachoendelea katika suala zima la uhifadhi wa mazingira.

Amesema hayo wilayani Hai mkoani Kilimanjaro Aprili 3, 2024 wakati wa ukaguzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwa pamoja na kuendelea na zoezi la upandaji miti kwenye maeneo mbalimbali.

“Upandaji wa miti ndio agenda moja wapo uliobeba ujumbe wa mbio za mwenge, hivyo lazima kila mmoja awe kielelezo katika utunzaji wa mazingira kwa kulinda na kuitunza miti tunayoipanda na kuhakikisha inakua na kuepuka uchomaji moto misitu.”

“Tunapokwenda kwenye halmashari na Mwenge wa Uhuru tukute tayari watu wameshapanda miti sababu hili sio jambo la kushtukiza na kumekuwa na baadhi ya halmashauri wanapouona mwenge ndio wanaandaa miti kwa ajili ya viongozi kupanda jambo ambalo sio sahihi,” amesema Bw. Mnzava.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Hai, Bw. Amir Mkalipa amesema kwa upande wao hadi sasa tayari wameshapanda miti milioni 1.2 kati ya 1.5 inayotakiwa kupanda kwa mwaka, hivyo miti 300,000 iliyosalia watatekeleza kabla ya mwaka kumalizika.

“Kwa Wilaya yetu ya Hai nikuhakikishie tutafikia lengo la maelekezo ya Makamu wa Rais ya kupanda miti milioni 1.5 kwa mwaka sababu zoezi hilo nalisimamia mwenyewe,” amesema Mkalipa.

Miti milioni 1.3 iliyopanwa Wilaya ya Hai kati ya hiyo 821 imepandwa katika Shule ya Sekondari ya Saashisha, 1,200 katika chanzo cha maji cha Njoro na miti 120 imepandwa katikaZahanati ya Kimashuku.

Settings