Katibu Mkuu Maganga awapa kongole waratibu miradi Ofisi ya Makamu wa Rais

Jan, 26 2024

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga amewapongeza waratibu wa miradi na mikataba inayoratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kwa juhudi wanazofanya katika utekelezaji wake.

Ametoa pongezi hizo katika kikao cha uwasilishwaji wa taarifa za Mikataba, Itifaki za Kimataifa na Kikanda zinazoratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Idara ya Mazingira kilichofanyika jijini Dodoma.

Bi. Maganga amesema kuwa juhudi na ushirikiano ni jambo muhimu katika kufanikisha lengo la kutimiza miradi yote inayosimamiwa kwa kuwa ni kazi kubwa inayofanywa na kila mmoja.

“Hizi ni kazi kubwa na ngumu hivyo mmejitahidi kusimamia vyema, najua changamoto hazikosekani hivyo lazima tujitahidi ili tuwe na mwongozo na mwisho wa siku tuongee lugha moja,” amesema Bi. Maganga.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Kemilembe Mutasa amesema kila mmoja ameona umuhimu wa mikataba pamoja na kuwa mwanachama.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais inatekeleza na kuratibu shughuli ya Hifadhi na Usimamizi Mazingira kwa manufaa mapana ya kitaifa kwa kizazi hiki na kijacho.

Aidha, katika utekelezaji wa shughuli hizi Serikali imekuwa ikitekeleza majukumu yake kitaifa na kimataifa ambapo kimataifa ni mwanachama wa Mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda.

Hivyo, Ofisi ya Makamu wa Rais ina wajibu wa kuratibu utekelezaji wa Mikataba na Itifaki hizi ikiwa pamoja na kuandaa kuratibu taarifa za utekelezaji wake, ushiriki katika mikutano mbalimbali na kuratibu utekelezaji wa miradi chini ya mikataba.

Settings