Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Mary Maganga ameupongeza uongozi wa Kituo cha Sayansi na Mazingira (CSE) cha nchini India kwa kuendeleza ushirikiano na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) katika kujenga uwezo na uzoefu katika masuala ya usimamizi na uhifadhi wa mazingira nchini.
Ametoa pongezi hizo alipokutana na ujumbe wa kituo hicho ulioongozwa na Mkurugenzi wa Programu Bw. Atin Biswas, jijini Dodoma.
Bi. Maganga amesema suala la usimamizi na uhifadhi wa mazingira linahitaji uelewa na kuimarisha mifumo ya kitaasisi kwa Mamlaka za Udhibiti wa Mazingira na kuongeza kuwa ushirikiano huo umekuja katika kipindi muafaka.
“Ziara hii ni kielelezo cha kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu baina ya Tanzania na India kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo hususani miradi ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira inayolenga kuleta manufaa kwa wananchi wetu," amesema Bi. Maganga.
Kwa upande wake Bw. Biswas ameipongeza Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais na NEMC kwa juhudi kubwa inazoendelea kufanya katika kusimamia Sheria ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira nchini.
"Tumekuwa na ushirikiano mkubwa na NEMC katika kujenga uwezo wa kitaasisi na kuendeleza mafunzo na tafiti na kuona namna tunavyoweza kushirikiana katika ukusanyaji taka ngumu na kuzihifadhi" amesema Biswas.
Naye Mkurugenzi Tafiti za Mazingira kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dkt. Menan Jangu amesema ziara hiyo imelenga kuimarisha maeneo muhimu ya vipaumbele vya miradi ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira inayotekelezwa kwa ushirikiano baina ya taasisi na Serikali.
Kituo cha CSE kilisaini makubaliano ya ushirikiano na NEMC na kujenga uwezo wa kiufundi, utafiti na ukaguzi wa tathmini ya athari ya mazingira katika maeneo ya Tanzania.