Katibu Mkuu Luhemeja ahimiza watumishi kuutangaza Muungano

Apr, 09 2024

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cypran Luhemeja amewahimiza watendaji wa Ofisi ya Makamu wa Rais kuendelea kuutangaza Muungano na kutoa elimu ya hifadhi ya mazingira.

Ametoa rai hiyo wakati wa kikao baina yake na Viongozi na Watendaji Waandamizi wa Ofisi hiyo kilichofanyika muda mfupi baada ya kuwasili rasmi katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma kuanza kutekeleza majukumu yake ya kazi Aprili 8, 2024.

Mhandisi Luhemeja amesema Muungano ni tunu muhimu kwa Watanzania na hivyo ipo haja ya wananchi kufahamu vyema historia yao na kutokana na umuhimu huo, mikakati mahsusi haina budi kuwekwa ili kuhakikisha makundi yote katika jamii yanafahamu na kuelewa Misingi, Chimbuko na Historia ya Muungano.

“Kuna Wizara 26 ndani ya Serikali, lakini jukumu la kutangaza Muungano tumepewa Ofisi ya Makamu wa Rais hususani katika kipindi hiki ambacho Muungano wetu unafikisha miaka 60 tangu kuasisiwa kwake, tunapaswa kuwa na mikakati ya ubunifu iliyo endelevu katika kutoa elimu kwa umma” amesema Mhandisi Luhemeja.

Amesema mkakati huo ujumuishe utoaji wa elimu kupitia makongamano na midahalo mbalimbali itakayojenga taswria chanya kwa Watanzania kuweza kufahamu fursa na manufaa ya muungano kwa faida ya vizazi vya sasa na vya baadae.

Kuhusu Hifadhi na Usimamizi Mazingira, Mhandisi Luhemeja amesema mafanikio makubwa yameendelea kupatikana akisisitiza juhudi na msukumo mkubwa zaidi unahitajika katika kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira ikiwemo suala la upandaji miti.

“Tunapaswa sasa kuja na mkakati mahsusi wa kuhakikisha jamii inajenga utamaduni wa kuhakikisha kila mtu anapanda pale anapokata mti kwani kwa kufanya hivi kutasaidia kukabiliana na madhara ya uharibifu wa mazingira” amesema Mhandisi Luhemeja.

Akifafanua zaidi Mhandisi Luhemeja amewataka viongozi na watendaji hao kufanya kazi kwa juhudi na maarifa kwa kujiwekea malengo na vipaumbele vinavyoweza kupimwa na kutekelezeka.

kikao hicho kilihudhuriwa na viongozi na watendaji mbalimbali wa Ofisi ya Makamu wa Rais akiwemo Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Bw. Abdallah Hassan Mitawi, Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Bi. Christina Mndeme na Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dkt. Immaculate Sware.

Itakumbukwa kuwa kabla ya kuhamia Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Luhemeja alikuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu).

Settings