Jamii yatakiwa kuhamasika katika upandaji wa miti

Jan, 28 2024

Jamii imeaswa kuhamasika katika upandaji miti na utunzaji mazingira pamoja na kupeana elimu juu ya mazingira kuanzia nyumbani, taasisi, vikundi shuleni na klabu za mazingira ili kuifanya nchi kuwa na mazingira mazuri.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP), Prof. Hozen Mayaya kwa niaba ya Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba katika zoezi la upandaji miti eneo la Miyuni Kaskazini jijini Dodoma leo Januari 28.

Amewapongeza waratibu wa kitaifa kwa Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kuadhimisha tukio hili adhimu kwa kupanda miti kwa lengo la kuhifadhi mazingira.

“Miti ni chanzo cha uhai, mbali na kupata hewa safi vilevile inatupatia matunda, kivuli na tiba. Hivyo kupanda kwetu miti hii ni ishara ya kuutakia Muungano wetu uhai ili udumu miaka mingi zaidi,” amesema Prof. Mayaya.

Ameongeza kuwa pamoja na faida hizo pia zoezi hilo lina lenga kuifanya jamii kujenga utamaduni wa kushirikiana katika kutunza mazingira, hivyo ameiasa jamii kutambua kuwa suala la uhifadhi wa mazingira linamuhusu kila mtu.

“Katika hili niombe jamii kuwa macho na mtu ambaye kwa njia moja au nyingine huaribu mazingira, tusimwonee haya na tumzuie asiharibu mazingira,” amesema.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Kemilembe Mutasa amesema Ofisi hiyo imeamua kuendesha zoezi hili mwezi huu kulingana na hali ya hewa ambayo kwa sasa inaruhusu kupanda miti ili itakapofika Aprili 26,2024 iwe siku ya kusherehekea.

Pia, Bi. Kemilembe amesema kuwa changamoto za mazingira ni nyingi ambazo ni mabadiliko ya tabianchi na athari zake zimeanza kuonekana na jitihada zimeanza kuchukuliwa.

Ameongeza Tanzania tayari imeweka mipango ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi huku Mkoa wa Dodoma ukiwekwa mahususi ambapo Ofisi ya Makamu wa Rais ndio inaratibu mpango huo nchini.

Settings