Jafo: Serikali yaongeza ubunifu kukabili mabadiliko ya tabianchi

Nov, 27 2021

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo amesema kuwa Serikali imeongeza ubunifu katika kukabilina na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi.

Jafo alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza wakati akichangia mada katika mjadala kuhusu mabadiliko ya tabianchi, athari na jitihada za Serikali katika kukabiliana nazo uliofanyika kwa njia ya mtandao.

Waziri Jafo alibainisha kuwa ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, asilimia 32 ya ardhi ya Tanzania imehifadhiwa kwa ajili ya kutumika katika masuala mbalimbali yanayohusu mabadiliko ya tabianchi.

Alisema hatua ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kushiriki mikutano mikubwa ya mazingira imesaidia nchi kupatiwa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kuzuia athari za mabadiliko ya tabianchi.

Waziri Jafo alitolea mfano Mkutano wa 26 wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP26) uliofanyika hivi karibuni mjini Glasgow, Scotland umevutia wadau mbalimbali ambao wameonesha nia ya kushiriki katika mapambano dhidi ya changamoto ya mabadiliko ya tabianchi.

Miradi mbalimbali rafiki kwa mazingira inatekelezwa hapa nchini kwa mfano Reli ya Kisasa (SGR), Mabasi ya Mwendo kasi (DART) na mbadala, kampeni ya upandaji miti ndo maana tunaelekeza kupanda miti milioni 1.5 kwa kila halmshauri kila mwaka yote hii ni jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” alisema.

Akiendelea kuchangia mjadala huo alisisitiza kuwa Serikali imepanga kuwalinda wananchi na kuhakikisha hawaathiriki na athari hizo kwa kuweka mikakati ikiwemo sera mbalimbali zinazosaidia kuzuia uharibifu wa mazingira.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Andrew Komba alisema kuwa Tanzania imepokea Sh. bilioni 650 kutoka Mifuko mbalimbali ya Mazingira ikiwemo GCF, GEF, AF na LDSF ambazo zitasaidia katika kutekeleza miradi mbaoimbali.

Alisema zipo nchi mbalimbali duniani zinazoshirikiana na Tanzania katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi zikiwemo Marekani, Uingereza, Norway, Denmark, Sweden, Japan na Korea Kusini.

Settings