Habari
Dkt Muyungi: Tanzania kuimarisha soko la biashara ya kaboni kimataifa
Tanzania imedhamiria kuongeza ushiriki wake kikamilifu katika soko la kimataifa la biashara ya kaboni huku Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) kikipewa jukumu la kuimarisha usimamizi, kuvutia uwekezaji wa kijani na kuongeza manufaa ya rasilimali za asili.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi ametoa kauli hiyo Julai 21, 2016 jijini Dar es Salaam kwenye kikao cha kwanza cha Bodi ya Wakurugenzi ya NCMC kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Alisema Tanzania inapaswa kubadilika kutoka kuwa mshiriki wa kawaida katika biashara ya kaboni na kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa kujenga mifumo thabiti itakayowezesha utekelezaji wa miradi ya kaboni yenye uadilifu wa hali ya juu.
Sanjari na hilo, Dkt. Muyungi alisisitiza kuwa ukuaji wa uchumi wa biashara ya kaboni duniani ni fursa muhimu kwa Tanzania kuongeza mapato ya Taifa huku likikabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Alisema soko la kaboni duniani linaendelea kukua kwa kasi na sasa linakadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 107 kwa mwaka, huku Afrika ikiwa na uwezo wa kuzalisha takribani dola bilioni 6 kwa mwaka ifikapo 2030 endapo itatumia kikamilifu fursa zilizopo.
Dkt. Muyungi alisema Tanzania ina nafasi kubwa ya kunufaika kutokana na utajiri wa rasilimali zake ikiwemo misitu, maeneo oevu, mifumo ya ikolojia ya pwani na bahari, pamoja na fursa zilizopo katika nishati safi na kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi.
Pia, alieleza kuwa hadi sasa Tanzania imesajili miradi 99 ya kaboni, huku zaidi ya mikopo ya kaboni milioni 13.4 ikiwa imetolewa ingawa mafanikio hayo bado hayajaakisi thamani halisi ya kiuchumi inayoweza kupatikana kupitia sekta hiyo.
Katibu Mkuu huyo aliongeza kuwa usimamizi madhubuti wa sekta ya kaboni utachangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuongeza mapato ya Serikali, kuvutia uwekezaji wa kijani, kuimarisha ustahimilivu wa jamii dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kuchochea maendeleo endelevu.



