Habari
Dkt. Muyungi aongoza wananchi kutunza mazingira Mbeya
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi, amewataka wananchi nchini kuendelea kudumisha utamaduni wa kupanda miti kama sehemu muhimu ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira, akieleza kuwa upandaji miti una mchango mkubwa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kuhifadhi vyanzo vya maji, kuboresha hali ya hewa pamoja na kuongeza uoto wa asili katika maeneo mbalimbali nchini.
Dkt. Muyungi ametoa wito huo leo Mei 24, 2026, alipokuwa akiongoza zoezi la upandaji miti katika viwanja vya Shule ya Msingi Tembela, iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, jijini Mbeya. Amesema kuwa ushiriki wa wananchi katika shughuli za mazingira ni hatua muhimu ya kuhakikisha taifa linakuwa salama kimazingira kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Amefafanua kuwa zoezi la upandaji miti linaenda sambamba na kampeni ya usafi wa mazingira inayoendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali ikiwa ni maandalizi kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani 2026, ambayo kitaifa yatafanyika jijini Dodoma tarehe Juni 5, 2026. Maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Center na kuhudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Aidha, amesema maadhimisho ya mwaka huu yamebeba kaulimbiu isemayo “Dira 2050: Tuwajibike Kukijanisha Tanzania”, ambayo inalenga kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika shughuli za utunzaji wa mazingira, ikiwemo upandaji miti, usimamizi wa taka, matumizi sahihi ya rasilimali za asili na kuendeleza mazingira safi na salama.
Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Lodrick Mpogolo, alimshukuru Dkt. Muyungi kwa kuchagua Mkoa wa Mbeya kuwa sehemu ya utekelezaji wa kampeni hiyo ya mazingira, akisema hatua hiyo imeongeza hamasa kwa wananchi na viongozi wa mkoa huo kushiriki kikamilifu katika shughuli za usafi na upandaji miti.
Bw. Mpogolo alisema Mkoa wa Mbeya umejipanga kuendelea kuimarisha utunzaji wa mazingira kupitia kampeni endelevu za usafi pamoja na upandaji miti katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo. Alibainisha kuwa mkoa umeweka malengo ya kupanda miti milioni 10.5 katika kipindi cha miaka 10 ijayo, kuanzia mwaka huu, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza uoto wa asili na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Katika hatua nyingine, Dkt. Muyungi aligusia maadhimisho ya kutimiza miaka 40 ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), yanayotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam tarehe Mei 29, 2026.
Amesema maadhimisho hayo ni sehemu ya kutathmini mafanikio yaliyopatikana katika usimamizi wa mazingira nchini pamoja na kuangazia mwelekeo wa taifa katika kukabiliana na changamoto za kimazingira.



