Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa madereva wanaoshiriki katika mfumo wa M- mama kuwahudumia akina mama wajawazito pamoja na watoto kwa staha, huruma na upendo pale wanapowasafirisha kutoka katika maeneo mbalimbali kuelekea katika vituo vya afya.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akizindua Mfumo wa Kurahisisha Usafiri wa Dharura kwa Mama Wajawazito na Watoto wachanga wa M- Mama kwa Mkoa wa Arusha katika hafla iliofanyika Hospitali ya Mount Meru leo tarehe 22 Juni 2023. Aidha ametoa rai kwa wale wote wanaohusika na usajili wa akina mama wajawazito kuhakikisha wanatekeleza jukumu hilo kwa ufasaha na kuzingatia namba ya dharura ya simu (115) inafahamika kwa kubandikwa sehemu mbalimbali ili wananchi waweze kuifahamu kirahisi.
Halikadhalika Makamu wa Rais amesema mfumo wa M-mama utakapoenea nchi nzima utawezesha kutimiza malengo ya kitaifa na kimataifa ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vya watoto wachanga huku akihimiza elimu kuendelea kutolewa kwa wananchi kwa kuwahamasisha wanawake wanahudhuria kliniki muda wote wa ujauzito na kujifungua katika vituo vya kutolea huduma ya afya.
Makamu wa Rais amesema serikali itaendelea kuboresha upatikanaji wa huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto na kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga. Ameongeza kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea na jitihada ya kuongeza idadi ya vituo vya kutolea huduma za Afya vinavyotoa huduma kamili za dharura na upasuaji ambapo hadi kufikia mwaka 2022 Serikali imeongeza vituo vya Afya zaidi ya 500 kutoka vituo vya Afya 155 mwaka 2017/18 pamoja na kuongezeka vituo vinavyotoa huduma za watoto wachanga (NICU) kutoka 14 mwaka 2018 hadi vituo 165 mwaka 2022.