Dkt. Mpango: Viongozi wa dini kemeeni mafundidho potofu

Sep, 10 2023

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa viongozi wa dini hapa nchini kutumia fursa ya teknolojia ya habari na mawasiliano kukemea mafundisho potofu na kufanya uinjilishaji wa neno la Mungu la kweli.

Makamu wa Rais ametoa wito huo leo tarehe 10 Septemba 2023 alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Ibada ya Jubilei ya Miaka 125 ya Uinjilishaji Jimbo la Iringa na Miaka 50 ya Upadre ya Mhashamu Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa iliofanyika katika Viwanja vya Kichangani Kanisa Kuu Jimbo Katoliki Iringa. Amesema ni muhimu kuendelea kuwahimiza waamini kufanya kazi kwa bidii huku wakimuomba Mungu abariki kazi za mikono yao na akili zao na kuwaepusha na baadhi ya viongozi wa dini ambao wamekuwa wakiwaelekeza waamini wao kuomba na kusubiri miujiza ili wapate mali bila kufanya kazi stahiki.

Aidha Makamu wa Rais amewasihi viongozi wa dini kukemea baadhi ya wahubiri ambao wamekuwa kwa uwazi na bila kificho wakishabikia matendo maovu kama ya ushoga na usagaji. Amesema ni vema Kanisa na madhehebu mengine kutambua jukumu kubwa la kuendelea kufundisha maadili mema katika jamii kwa nguvu na maarifa zaidi ili kuwa na Taifa salama sasa na baadae. Makamu wa Rais amesema kutokana na mmomonyoko wa maadili matendo maovu yameongezeka ikiwemo unyanyasaji wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto na wanawake, ongezeko la familia za mzazi mmoja, ongezeko la watoto waliozaliwa nje ya ndoa, migogoro ya ndoa, ongezeko la talaka, migogoro ya mirathi, vitendo vya ushoga na ulawiti.

Makamu wa Rais ametoa wito kwa kanisa kuendelea kuwasaidia wahitaji katika jamii hususan watoto yatima, watu wenye ulemavu, masikini, wajane, wafungwa na wenye shida mbalimbali. Aidha ametoa rai kwa waamini wa dini zote kujenga tabia ya kusaidia watu wenye uhitaji katika jamii na kuepuka kujilimbikizia mali isivyo halali.

Halikadhalika Makamu wa Rais amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa Kanisa Katoliki katika kumwinua na kumstawisha mwanadamu kiroho na kimwili. Ameongeza kwamba Katika miaka 125 ya uinjilishaji, Kanisa Katoliki katika Jimbo la Iringa limekuwa likishughulikia ustawi wa jamii kama vile kuimarisha upatikanaji wa huduma mbalimbali za jamii hususan afya na elimu. Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na madhehebu yote ya dini nchini katika kuwaletea watanzania maendeleo na kudumisha haki na amani katika Taifa.

Vilevile Makamu wa Rais ametoa rai kwa viongozi wa dini na waamini wa dini zote kuzingatia mafundisho ya imani hususani kuhusu wajibu wa kuitunza vema dunia tuliyokabidhiwa na Mwenyezi Mungu. Amesema watanzania wote wanapaswa kutambua kuwa jitihada za Serikali katika kukabiliana na athari za uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi hazitafanikiwa kama wananchi wote hawatabadili tabia na kuchukua hatua za makusudi kulinda na kuhifadhi mazingira.

Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Iringa Mhashamu Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa amewashukuru waamini, viongozi pamoja na wote naoshirikiana nao katika uongozi wake wa kanisa mkoani Iringa.

Settings