Dkt. Mpango: Tumuenzi Baba wa Taifa kwa kufanya kazi kwa bidii

Oct, 14 2023

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Watanzania kumuenzi Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuboresha Maisha pamoja na kuinua uchumi wa Taifa.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akizungumza kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Misa Maalum ya Kitaifa ya Kumuombea Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Roho Mtakatifu – Babati mkoani Manyara. Amewasihi viongozi na watanzania kwa ujumla kumuenzi Baba wa Taifa kwa kuishi katika misingi ya kukemea rushwa, kupiga vita umasikini, kutojilimbikizia mali pamoja na kukemea matendo mabaya.

Makamu wa Rais amesema ni wajibu kwa watanzania kumuenzi kwa kuishi maisha aliyoishi Baba wa Taifa kwa kuwa alitumia elimu na vipaji vyake kwa faida ya wote, alithamini dhamana aliyopewa, alikuwa mnyenyekevu na mwenye kujisahihisha alipokosea. Ameongeza kwamba alikemea matendo mabaya yaliochochea mmomonyoko wa maadili, alikuwa mwanamazingira hodari na alipiga vita umasikini.

Aidha Makamu wa Rais amelishukuru Kanisa pamoja na taasisi zingine za kidini kwa ushirikiano wake na Serikali kwa kutoa huduma mbalimbali za kijamii kama vile elimu, afya, mazingira na mengineyo. Amesema serikali itaendelea kushirikiana vema na kanisa katoliki pamoja na madhehebu yote ya dini katika kuwatumikia watanzania. Halikadhalika Makamu wa Rais amewasihi viongozi wa dini kuendelea kuliombea taifa amani na utulivu.

Misa Maalum ya Kitaifa ya Kumuombea Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere imeongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Mbulu Anthony Lagwen na kuhudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Viongozi mbalimbali pamoja na waumini kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Settings