Dkt. Mpango: Tanzania, Cuba zakubaliana kuongeza ushirikiano

Jan, 24 2024

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema Tanzania na Jamhuri ya Cuba zimekubaliana kuongeza ushirikiano katika sekta mbalimbali za kipaumbele kama vile elimu, afya, kilimo na utalii.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akizungumza na vyombo vya habari kuhusu mazungumzo waliyofanya na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Cuba Mhe. Salvador Valdés Mesa Ikulu Jijini Dar es salaam. Amesema katika mazungumzo hayo wamekubaliana kuimarisha Tume ya Kudumu ya Pamoja kwa lengo la kushirikiana kimkakati katika namna ya kuibua fursa mbalimbali na kuziendeleza.

Pia Makamu wa Rais Dkt. Mpango amesema Jamhuri ya Cuba imeridhia kuongeza watalaam wa afya kwa pande zote Tanzania bara na Zanzibar. Ameongeza kwamba Tanzania imedhamiria kuiunga mkono Cuba katika adhma yake ya kufanya kongamano la kuendeleza lugha ya Kiswahili nchini Cuba pamoja na nchi za kusini mwa Amerika la mwaka 2024.

Halikadhalika Makamu wa Rais amesema kupitia Wizara za Afya za Tanzania na Cuba zitashirikiana katika kuhakikisha Kiwanda cha kuzalisha dawa na kuua vimelea vya ugonjwa wa Malaria kilichopo Kibaha mkoani Pwani kinaendelea kuzalisha kulingana na uwezo wake. Amesema serikali hizo zitashirikiana katika kuwezesha kiwanda hicho kuzalisha bidhaa zaidi ya kumi ambazo kiwanda hicho kinaweza kuzalisha pamoja na kutafuta masoko ya bidhaa hizo katika nchi Jirani na zinginezo.

Makamu wa Rais amesema Mazungumzo yao yalilenga kuimarisha zaidi ushirikiano ulioasisiwa na waanzilishi wa mataifa hayo ulioanza mwanzoni mwa miaka ya 1960.

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Cuba Mhe. Salvador Valdés Mesa ameishukuru serikali ya Tanzania kwa ushirikiano uliopo na Cuba pamoja na kuendelea kuiunga mkono nchi hiyo katika kukemea vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa kwa miaka 60 hivi sasa.

Amesema nchi ya Cuba inaendelea na jitihada za kujiletea maendeleo ambapo kwa sasa imepiga hatua katika masuala mbalimbali ya teknolojia ikiwemo uzalishaji wa dawa adimu duniani. Amesema ushirikiano unaoendelea na Tanzania ikiwemo kusainiwa kwa hati za Makubaliano za kushirikiana katika masuala ya vyuo vikuu pamoja na sekta ya dawa na vifaa tiba kutatoa fursa kwa Tanzania kupata dawa zenye viwango vya juu kutoka mamlaka za Cuba.

Tanzania na Cuba zimekuwa zikishirikiana katika masuala mbalimbali ya kitaifa, kikanda na kimataifa. Cuba ilifungua Ubalozi wake hapa nchini mwezi Februari 1964 na Tanzania ilianzisha Ubalozi wake nchini Cuba Aprili 2019. msingi imara wa uhusiano wa kihistoria baina ya Tanzania na Cuba ulijengwa na kuimarishwa zaidi na mahusiano ya viongozi wa nchi hizo mbili yaani Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Kamanda Fidel Castro Ruz na baadaye kuendelezwa na kudumishwa na viongozi waliofuata wa mataifa haya mawili.

kwa ngazi ya kimataifa, Tanzania na Cuba zimeendelea kushirikiana kwa kuwa na msimamo wa pamoja zikionesha mshikamano katika masuala yenye maslahi ya pamoja kwa pande zote mbili. Mataifa yote mawili ni wanachama hai wa umoja wa nchi zisizofungamana na upande wowote (NAM), nchi za kundi la G77+China na yanaunga mkono mfumo wa usawa wa kiuchumi wa kimataifa na uwepo wa demokrasia ya kweli kwenye Umoja wa Mataifa na ni wafuasi wa Ushrikiano wa kusini yaani South-south Cooperation.

Settings