Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema serikali itaendelea kuboresha sekta ya afya nchini kwa kuongeza bajeti ili ili kuongeza tija katika kutoa huduma bora za afya kwa wananchi.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akiwa ziarani mkoani Ruvuma katika uzinduzi wa Kituo cha Afya Lilambo kilichogharimu shilingi milioni 503 kilichopo Manispaa ya Songea mkoani humo. Amesema jitihada zinaendelea katika kuongeza vifaa tiba, kusomesha watalaamu wa afya pamoja na kuongeza magari ya kubeba wagonjwa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchi nzima.
Makamu wa Rais amewataka wananchi wa Lilambo kutumia vema kituo hicho cha afya kwa kulinda miundombinu yake. Aidha amewaagiza viongozi na watoa huduma kuhakikisha vifaa tiba vinafanyiwa ukarabati kwa wakati pamoja na kudhibiti utoroshaji wa dawa kutoka vituo vya kutolea huduma kwenda maduka binafsi.
Pia amewapongeza watoa huduma za afya kwa kuendelea kujitoa kufanya kazi hiyo na kuwaasa kuzingatia maadili sheria na taratibu za taaluma hiyo wakati wote wa kazi. Amesema wananchi hutegemea zaidi msaada wa watoa huduma za afya pale wanapopata changamoto za kiafya hivyo ni vema kuendelea kutumia lugha zenye staha na ufariji kwa wagonjwa hususani mama wajawazito wanapojifungua.
Makamu wa Rais ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Ruvuma kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa kituo cha Afya Lilambo pamoja na kuwapongeza madiwani kwa uamuzi wao wa kutoa mapato ya halmashauri takribani shilingi milioni 500 kukamilisha kituo hicho.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amewasihi viongozi wa mkoa wa Ruvuma kusimamia vema fedha za miradi zinazopelekwa mkoani humo ili kupata miradi bora itakayowasaidia wananchi kwa muda mrefu. Pia ametoa tahadhari kwa wote wanaotumia utaratibu wa serikali kutoa pembejeo za kilimo kujinufaisha wao binafsi kuacha mara moja tabia hizo.
Halikadhalika Makamu wa Rais amewaasa wananchi wa mkoa wa Ruvuma kutunza na kudumisha amani iliopo kwa kuwa macho na viashiria vya uvunjifu wa amani na kutoa taarifa.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais -TAMISEMI Deogratius Ndejembi amesema Serikali katika mwaka wa fedha 2023-2024 imetenga zaidi ya shilingi bilioni 115 kwaajili ya ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa zaidi kwa lengo la kuboresha utoaji huduma za afya nchini. Pia amesema takribani shilingi bilioni 916 zimetengwa kwaajili ya ununuzi wa mgari ya kubeba wagonjwa ambapo manispaa ya Songea inatarajia kupata magari mawili.
Ndejembi amesema Serikali itahakikisha inatekeleza ujenzi wa Wodi mbili zinazohitajika katika kituo cha Afya Lilambo pamoja kutoa shilingi milioni 100 zilizopangwa kwaajili ya vifaa tiba katika kituo hicho.