Dkt. Mpango: Serikali imedhamiria kuboresha uzalishaji katika kilimo

Aug, 20 2024

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuboresha na kuinua uzalishaji katika kilimo na kupunguza upotevu wa mazao baada ya kuvunwa.

Makamu wa Rais amesema hayo mara baada ya kuweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Kituo Mahiri cha Usimamizi wa Mazao ya Nafaka ambacho kitatumika kudhibiti sumu kuvu kilichopo eneo la Mtanana Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma. Amesema ujenzi wa kituo hicho ni suluhisho la changamoto za muda mrefu zilizokuwa zikiwakabili wakulima pindi mazao yao yanapozuiliwa katika masoko kutokana na tatizo la sumu kuvu.

Ameipongeza Wizara ya Kilimo kwa kutoa mafunzo ya mbinu bora za kilimo katika kupambana na sukumuvu mkoani Dodoma ambapo jumla ya Wakulima 12,517 wamepatiwa mafunzo kupitia mradi huo na kuitaka Wizara kuendelea kutoa elimu ya kilimo bora kwa wakulima.

Makamu wa Rais ameielekeza Wizara ya Kilimo kupitia Wakala wa Mbegu (ASA) kuhakikisha upatikanaji wa mbegu bora na zenye bei nafuu kwa wakulima pamoja na kufanya udhibiti wa mbegu feki kwa kukagua wauzaji na wazalishaji wa mbegu hizo.

Aidha akiwa katika ziara hiyo Wilaya ya Kongwa, Makamu wa Rais ameagiza Wizara ya Kilimo kupitia Tume ya Umwagiliaji kufanyia kazi ombi la wananchi wa Mtanana kuhusu bwawa la umwagiliaji litakalosaidia kuondoa adha ya mafuriko ya mara kwa mara katika eneo hilo pamoja na kukuza kilimo kwa njia ya umwagiliaji.

Ameiagiza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Bodi za Nyama na Maziwa kuangazia uonevu na utapeli katika biashara ya mifugo hususan ng’ombe Wilayani Kongwa. Amesema Mazingira ya soko la mifugo na mazao ya mifugo ni lazima liwe la haki na lenye uhalisia kwa kuhakikisha mauzo yanafanyika kwa kutumia vipimo halali badala ya kukadiria.

Halikadhalika ametoa wito kwa Taasisi za utafiti ikiwemo TARI kuangazia mazao mapya yanayoweza kustawi mkoani Dodoma kwa kuwa ardhi hiyo ina fursa ya kuzalisha mazao mengi.

Amewataka Viongozi wakiwemo Mawaziri na Naibu Mawaziri, Wakuu wa Mikoaa na Wilaya kupunguza muda wa kukaa ofisini na badala yake kuwatembelea wananchi ili kutatua changamoto zinazowakabili.

Kwa upande wake Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe amesema mradi wa kituo Mahiri cha Usimamizi wa Nafaka unahusisha kiwanda cha kuchakata unga ambapo Wizara imedhamiria kuongeza mitambo ya kuchanganya virutubisho na kuepusha changamoto zinazojitokeza za hitajio la kuchanganya virutubisho nje ya nchi.

Bashe ameongeza kwamba Kiwanda kilichopo katika kituo hicho kitaruhusu wakulima wadogo kutumia kuchakata mahindi yao kwa gharama nafuu zaidi na kuwauzia wateja wao. Aidha amesema Wizara itatengeneza utaratibu mpya wa usimamizi wa mbegu za mahindi ili kuondoa mbegu feki.

Amesema Wizara haitasita kufuta leseni za wazalishaji wa mbegu ikiwa mawakala wao watatumia majina ya mbegu hizo kuuza mbegu feki sokoni.

Awali Makamu wa Rais akiwa ziarani Wilaya ya Mpwapwa amezindua Shule ya Sekondari ya Kimaghai “A” yenye jumla ya majengo 11 iliyogharimu shilingi milioni 544.2.

Shule hiyo inatarajiwa kupunguza umbali mrefu waliokuwa wakimbea wanafunzi wa vijiji vya Kimaghai na Inzomvu.

Settings