Dkt. Mpango awataka wahitimu Chuo cha Utumishi wa Umma kuzingatia maadili

Jun, 06 2024

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amewataka wahitimu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kuzingatia maadili, miongozo na kuheshimu mipaka ya kazi yao ikiwemo utunzaji wa siri ambazo watazifahamu katika utendaji kazi wao.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati aliposhiriki Mahafali ya 39 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam. Amesema kushindwa kutunza siri za Serikali kunadhoofisha ufanisi na kurudisha nyuma hatua za utekelezaji wa majukumu mbalimbali na wakati mwingine hupelekea uhasama kati ya watumishi na kuvuruga utendaji kazi na uhusiano mwema kazini.

Aidha Makamu wa Rais amewasihi wahitimu hao kuwa chachu ya mabadiliko kwa kufuata sheria, taratibu na kanuni, kuzingatia maadili na kuepuka mienendo isiyofaa. Amesema kwa sasa Utumishi wa umma unakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha na mali ya umma, matumizi mabaya ya ofisi za umma, kutowajibika na mmomonyoko wa maadili.

Vilevile Makamu wa Rais ametoa wito kwa Waajiri wote nchini kuzingatia maelekezo ya Waraka wa Utumishi wa Umma Namba 5 wa mwaka 2011 unaowataka waajiri katika Utumishi wa Umma kutenga fedha ili kuhakikisha watumishi wapya wote wanapatiwa mafunzo elekezi ya awali ndani ya kipindi cha miezi mitatu mara baada ya kuripoti kazini.

Pia Makamu wa Rais amesema Chuo cha Utumishi wa Umma kinapaswa kujipanga kutoa elimu itakayowajengea wahitimu uwezo wa kujiajiri na kuwa na ubunifu ambao utawasaidia kuchangamkia fursa zinazojitokeza. Amesema ni muhimu Chuo hicho kuhakikisha wakati wote kinatoa elimu inayoendana na mahitaji ya soko na mabadiliko ya teknolojia inayokua kwa kasi pamoja na vipaumbele vya kitaifa ikiwamo ujenzi wa uchumi wa viwanda, uchumi wa buluu, uchumi wa kidigiti, nishati jadidifu, na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Makamu wa Rais amesema Serikali imejipanga kuhakikisha sekta ya elimu inaboreshwa zaidi ili kukidhi mahitaji na kuendana na jitihada za kuleta maendeleo endelevu nchini. Ameongeza kwamba Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya Vyuo na kuongeza udahili ili wananchi zaidi wapate fursa ya kujiendeleza kimasomo.

Settings