Dkt. Mpango amuwakilisha Rais Samia Mkutano EAC

May, 31 2023

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amemwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Dharura wa 21 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika Ikulu ya Bujumbura nchini Burundi.

Mkutano huo umejadili hali ya usalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na kuridhishwa na juhudi zilizofanyika katika kuleta amani.

Pia umelipongeza Jeshi la Kikanda kwa jitihada zake za kurejesha amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pamoja na kumpongeza Raiswa DRC Felix Tshiseked kwa kukubali kuongeza muda wa miezi mitatu kwa Jeshi la Kikanda ili kuweza kusimamia vema mafanikio yaliopatikana.

Aidha, katika mkutano huo umefanyika uteuzi wa Naibu Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ikienda sambambana uteuzi wa Jaji wa Mahakama wa Divisheni ya Awali katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki.

Walioteuliwa na kuapishwa ni pamoja na Bi Annette Ssemuwemba Mutaawe kutoka Jamhuri ya Uganda ambaye atashika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Umoja wa Forodha, Biashara na Masuala ya Umoja wa Fedha pamoja na Bw. Andrea Aguer Ariik Malueth kutoka Jamhuri ya Sudan Kusini kushika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Masuala ya Miundombinu, Sekta za Uzalishaji, Kijamii na Siasa.

Pia umeteua na kumuapisha Mhe. Jaji Kayembe Kasanda Ignace Rene kuwa Jaji wa Mahakama ya Divisheni ya Awali ya Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki na kumteua Jaji Omar Othman Makungu kutoka nchini Tanzania kuwa Jaji wa Mahakama ya Afrika Mashariki.

Mkutano wa Dharura wa 21 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) umehudhuriwa na Wakuu wa Nchi akiwemo Rais wa Burundi ambaye ni Mwenyekiti wa EAC Mhe. Evariste Ndayishimiye, Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. William Ruto.

Pia Wawakilishi wa Wakuu wa Nchi ambao ni pamoja Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango, Waziri Mkuu wa Rwanda Mhe. Dkt. Edouard Ngirente, Naibu Waziri Mkuu wa Uganda na Waziri wa Masuala ya Afrika Mashariki Rebecca Kadaga, Waziri kutoka Ofisi ya Rais Sudan Kusini Mhe. Dkt. Barnaba Marial pamoja na Waziri wa Ushirikiano wa Kikanda wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Mhe. Antipas Nyamwisi.

Pia wengine waliohudhuria ni pamoja na Mawaziri wa Ulinzi, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na Wanadiplomasia.

Settings