Dkt. Kijaji: Utalii wa bahari ni matunda ya utunzaji mazingira

Aug, 24 2024

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema kuwa utalii wa bahari katika eneo la Zanzibar ni matunda ya utunzaji wa mazingira.

Kutokana na hali hiyo, Mhe. Dkt. Kijaji ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za utunzaji wa mazingira ikiwemo kupanda miti na kutoharibu vyanzo vya maji.

Amesema hayo wakati aliposhiriki katika hafla ya uzinduzi wa Utalii wa Kasa katika Pango la Salaam Kizimkazi Dimbani Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar leo Agosti 24, 2024 ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Zanzibar. Mhe. Mudrik Ramadhan Soraga, Dkt. Kijaji amesema utalii ni uchumi hivyo mazingira yakiendelea kutunzwa taifa litaendelea kuingiza fedha za kigeni.

Aidha, Dkt. Kijaji amewapongeza wawekezaji ambao wameona wameona fursa ya kuwekeza kwenye kivutio cha utalii ili kuvutia zaidi Kimzimkazi, Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

“Tumeelezwa hapa tayari Watanzania 16 wameajiriwa kwenye eneo hili kwa ajili ya kuhudumia watalii wa ndani na wa nje, hili ni eneo muhimu kwa Watanzania kwani tunakuza uchumi wa taifa letu,“ amesema.

Aidha, Waziri Dkt. Kijaji ameahidi kushirikiana na wadau wote katika kazi ya kutunza mazingira ili kuendelea kuzalisha vivutio vingi vya utalii ili kutengeneza fedha na hivyo kukuza uchumi

Hafla hiyo pia imehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis.

Settings