Dkt. Kijaji: Tutahakikisha Hoja za Muungano zilizosalia zinatatuliwa

Sep, 26 2024

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema katika kuhakikisha hoja za Muungano zilizosalia zinatatuliwa haraka, Ofisi ya Makamu wa Rais imetenga siku tatu kwa kila mwezi kwa ajili ya kushughulikia hoja hizo ikiwa ni pamoja na kutembelea miradi ya Mazingira inayotekelezwa kwa pamoja.

Dkt. Kijaji ameyasema hayo Ikulu, Zanzibar Septemba 25,2024 alipokuwa akizungumza na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi mara baada ya kwenda kujitambulisha huku akiwa ameambatana na timu ya Makatibu wakuu, Wakurugenzi na watendaji wengine.

Mhe. Dkt. Kijaji amesema Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kuweka mkazo katika kuzipitia Sera, kanuni miongozo, mipango na mikakati ya kudhibiti changamoto za mazingira na mabadiliko ya tabianchi.

Ameongeza, uvamizi wa majichumvi kwenye maeneo ya kilimo, visima na makazi ya wananchi, mporomoko wa fukwe za bahari na ukosefu wa mvua na mvua zisizotarajiwa bado ni matatizo yanayoathiri nchi kwa kiasi kikubwa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Kijaji amemtembelea Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ambapo alielezea kuhusu kuwepo kwa siku tatu kila mwezi kwa watendaji wa ofisi hiyo kukutana Zanzibar na kuwa na mikutano na wananchi kuhusu masuala ya Mazingira na Muungano.

“Uratibu wa shughuli za Muungano kwenye sekta zote tunazozisimamia zinahitaji ushirikiano wa karibu ili kuleta ufanisi na tumeandaa timu ya wataalamu na imeanza utafiti na kuandika miradi kwa lengo la kuiwasilisha kwa wafadhili ili kupata fedha zitakazoendesha miradi ya kimazingira.”

Ameongeza kuhusu biashara ya kaboni, kuna fursa kubwa kwa wananchi ambao wakipata elimu ya kutosha watanuifaika kutokana na uwepo wa misitu mingi lakini bado elimu juu ya suala hilo bado haijawafikia wengi.

Aidha amesisitiza juu ya utolewaji wa elimu ya Nishati safi ya kupigia huku akiwahamasisha wananchi kutunza Mazingira, kwani Mazingira ni uhai tuyatunze ili yatutunze na tukiyaharibu yatatuadhibu.

Settings