Dkt. Kijaji: Tanzania inajitahidi kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi

Sep, 02 2024

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema Tanzania imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali katika kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi kwa kupitisha sera na mipango mikakati ya kina.

Mhe. Dkt. Kijaji ameyasema hayo katika ufunguzi wa Mkutano wa 35 wa Kamati ya Kudumu ya Fedha ya Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) ulioanza leo Septemba 2, 2024 mkoani Arusha katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) ambapo mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango.

Amesema moja ya jitihada ni pamoja na kuwepo kwa Sera ya Kitaifa ya Mazingira (2021), Mpango Mkuu wa Kitaifa wa Masuala ya Kimkakati (2022-2032) pamoja na Sera ya Kitaifa ya Uchumi wa Buluu (2024).

“Ninawakaribisha nyote Arusha, Tanzania, ambayo mara nyingi huheshimika kama “The Geneva of Africa.” Kama mji mkuu halisi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Arusha ni ushuhuda wa dhamira yetu ya juhudi za ushirikiano katika kushughulikia changamoto za kikanda na kimataifa, na tunayo heshima kubwa kuwa mwenyeji wa mkutano huu muhimu wa Kamati ya Kudumu ya Fedha ya UNFCCC.

“Kwa niaba ya nchi mwenyeji, natoa shukrani zangu za dhati kwa Mwenyekiti na Wajumbe wa Kamati kwa kuipa Tanzania fursa ya kuwa mwenyeji wa mkutano huu muhimu,” amesema Mhe. Dkt. Kijaji.

Ameongeza kwa kumshukuru Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango kwa kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye alikubali kuwa mgeni rasmi wa mkutano huo.

“Lazima niipongeze kazi bora iliyofanywa na Kamati hya Mkutano wa UNFCCC na timu yetu ya Taifa iliyojitolea kwa maandalizi ya kina kuelekea katika mkutano huu.

Amesema ukweli ni kwamba mabadiliko ya tabianchi huleta athari kubwa, zinazojidhihirisha kupitia matukio mabaya ya hali ya hewa kama vile mafuriko, dhoruba, mvua zisizo na uhakika pamoja na uharibifu wa miundombinu.

Settings