Dkt. Jafo: Wakuu wa Mikoa simamieni ajenda ya mazingira

Aug, 26 2023

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo ametoa rai kwa wakuu wa mikoa kuifanya ajenda ya usafi wa mazingira kuwa ya kudumu.

Ametoa wito huo tarehe 26 Agosti, 2023 wakati akizungumza wakati wa Mafunzo ya Uongozi kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa yanayofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere iliyopo Kibaha mkoani Pwani.

Dkt. Jafo amewataka wakuu hao wa mikoa kuzielekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa zilizo chini yao kusimamia vyema zoezi la usafi wa mazingira katika maeneo yao ili kuifanya miji kuwa safi.

Alisisitiza kuwepo na utaratibu maalumu wa kujisaidia (kuchimba dawa) kwa abiria wanaosafiri kwa mabasi badala ya porini kama unavyofanyika kwa baadhi ya mabasi hali inayosababisha uchafuzi wa mazingira.

Aidha, Waziri Jafo aliwataka wakuu wa mikoa hao kusimamia suala la upangaji wa miji katika maeneo yao ili uwekezaji usikwame kutokana na changamoto za kimazingira.

Alisema kuwa bila kupanga miji vizuri uwekezaji unakuwa ni changamoto kubwa kwani itawalazima wawekezaji kusubiri kupata Cheti cha Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA) kabla ya kuanza hatua ya ujenzi wa miradi.

“Mtu atataka kujenga kiwanda katika makazi ya watu, mambo yanakuwa yanaingiliana na mwisho wa siku wakati mwingine EIA zinachelewa kwasababu tumeshindwa kufuata utaratibu wa mipango miji hivyo, tuwasisitize watu wetu wa mipango miji kuhakikisha wanapanga vizuri miji yetu kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi,” alisisitiza.

Kwa upande mwingine Waziri Dkt. Jafo aliwahimiza viongozi hao kuendelea kusimamia zoezi la upandaji wa miti milioni 1.5 kwa mwaka katika kila halmashauri wanazozisimamia ili hifahi ya mazingira iwe endelevu.

Settings