Dkt. Jafo: Vijana tumieni fursa za utunzaji mazingira

Oct, 22 2023

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dk. Selemani Jafo amewataka vijana kutumia fursa mbalimbali zitokanazo na utunzaji wa mazingira na kuokoa viumbe hai ili kujikwamua kiuchumi kupitia miradi mbalimbali ya kukabilina na mabadiliko tabianchi.

Amesema hayo wakati akifungia mkutano wa kujadili namna bora ya kutumia fursa mbalimbali zinazotokana na utunzaji wa mazingira ulioshirikisha vijana kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

Dkt. Jafo amesema bado kuna changamoto zinazoikumba sekta ya mazingira kutokana na mabadiliko tabianchi ambayo huathiri uhai wa viumbe hai na misitu hivyo amewataka vijana kutumia fursa za utunzaji wa mazingira kujiingizia kipato.

“Tunapoelekea Mkutano wa COP 28 unaotarajiwa kufanyika kule Dubai vijana mnatakiwa kutumia fursa zitakazojitokeza katika mkutano huo ili kujikwamua kiuchumi,“ amesema.

Waziri Jafo ameongeza baadhi ya takataka zimekuwa zikibadilishwa kuwa fursa kama magurugumu ya magari kutengeneza meza au viti vinavyoweza kutumika tena, makopo ya plastiki kutengenezea mapambo mbalimbali.

Hali kadhalika amebainisha kuwa baadhi ya vyuma chakavu vimekuwa vikitengeneza mapambo mbalimbali yanayotumika katika maeneo mbalimbali hivyo vijana hawana budi kutumia fursa hii.

Ametoa wito kwa vijana kuiokoa nchi isiingie kwenye jangwa kwa kufanya ubunifu wa vitu mbalimbali kama ambavyo Serikali imeweka kipaumbele kwa vijana katika kusaidia taifa kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake Mshauri wa Rais kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi Dk. Richard Muyungi amesema Rais Mhe. Dkt. Samia amekuwa ni kinara wa kupinga uchafunzi wa mazingira na kutoa baadhi ya maagizo kwa watenadaji mbalimbali kutafuta njia bora yakupambana na hali hiyo.

Katika kumuunga mkono Dkt. Muyungi amesema ni lazima watendaji kuhakikisha katika shughuli mbalimbali tunazofanya zizingatie usalama wa mazingira ikiwa ni pamoja na kupanda miti, kulinda vyanzo mbalimbali vya maji, kuzuia utupaji wa taka hovyo nakusisitiza wananchi kuacha kutupa taka hovyo.

Settings