Dkt. Jafo: Tanzania kupunguza uzalishaji wa gesijoto

May, 13 2022

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema Tanzania imepanga kupunguza uzalishaji wa gesi joto kwa asilimia 30 hadi 35 ifikapo mwaka 2030.

Pia ameyaomba mashirika ya kimataifa kuunga mkono jitihada za Tanzania katika kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kusaidia misaada ya kifedha ili kufanikisha jitihada hizo.

Dkt. Jafo amesema hayo Mei 12, 2022 wakati akihutubia Mkutano wa Mawaziri wa Nchi zinazotekeleza Miradi ya Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi chini ya ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Mitaji (UNCDF) kupitia Local Climate Adaptive Living Facility – Shirika la LoCAL uliofanyika jijini Brussels, Ubelgiji.

Alisema Tanzania inaathiriwa na mabadiliko ya tabianchi kwa kiwango kikubwa kama ilivyo katika mataifa mengi duniani ikiwemo kuongezeka kwa joto katika baadhi ya maeneo, ukame, kuvurugika kwa misimu ya mvua na mafuriko na kusababisha hasara kubwa za kijamii na kiuchumi katika sekta za kilimo, ufugaji, nishati, uvuvi na miundombinu.

Alitolea mfano katika kipindi cha muongo mmoja uliopita Tanzania ilipata hasara ya kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 96.6 katika sekta ya kilimo pekee kutokana na ukame.

Aidha, Waziri Jafo alieleza kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi zinaigharimu nchi kwa asilimia 1 hadi 3 ya Pato la Taifa ambapo kwa mujibu wa Benki ya Dunia hatua zisipichukuliwa mabadiliko ya tabianchi yatachangia ongezeko la umaskini kwa asilimia 2 hadi 3 ifikapo mwaka 2030.

Kwa upande wa Zanzibar alisema takriban asilimia 30 ya ardhi ipo chini ya wastani wa mita 5 juu ya usawa wa bahari, mabadiliko ya tabianchi yamesababisha baadhi ya visiwa kupotea kutokana na ongezeko la kina cha bahari, visima kuingiwa na maji ya chumvi na kuharibiwa kwa ardhi ya kilimo kutokana na maji ya chumvi kuvamiabaadhi ya maeneo.

“Juhudi kubwa zinahitajika kitaifa na kimataifa kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi hususan kwa kusaidia mataifa yanayoendelea kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi,” alisema Dkt. Jafo.

Hata hivyo alibainisha kuwa Tanzania imechukua hatu mbalimbali kukabiliana na kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo kuimarisha mifumo ya kitaasisi na kisera pamoja na kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi.

“Katika kukabiliana na tatizo la mabadiliko ya tabianchi, Tanzania imeweka kipaumbele katika utekelezaji wa miradi mikubwa yenye lengo la kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa ikiwemo Mradi wa Reli ya Kisasa (Standard Gauge Railway) ambayo itatumia umeme na hivyo kupunguza matumizi ya dizeli ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa hewa ya ukaa,” alibainisha.

Aliongeza kuwa Mradi wa Bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere (Mwalimu Nyerere Hydropower Plant) ambao ni chanzo cha nishati jadidifu (renewable energy) unaotarajiwa kuzalisha megawati 2,115 na utachangia matumizi ya dizeli na makaa ya mawe katika uzalishaji wa nishati hivyo kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa nchini.

Kwa mujibu wa Waziri Jafo, mradi mwingine wa Mabasi yaendayo Haraka (Dar es Salaam Bus Rapid Transit - BRT) ambao unapunguza idadi ya mabasi yanayotoa huduma na ambao unatarajiwa kutumia gesi asilia (LNG) badala ya dizeli.

Katika eneo la kuhimili athari mabadiliko ya tabianchi, alisema Tanzania inatekeleza Sera, Mikakati na Miradi mbalimbali inayolenga kuhimili athari mabadiliko za tabianchi katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo ujenzi wa kuta za bahari katika eneo la Barabara ya Barack Obama (Ocean Road) Dar es Salaam, Pangani, Pemba na Unguja kuzuia athari za ongezeko la kina cha bahari.

Alitaja miradi mingine ni ya kupanda miti na mikoko pamoja na kuwezesha jamii kufanya shughuli mbadala za kujipatia kipato katika maeneo yaliyoathirika zaidi.

Jafo alieleza pia Serikali inatekeleza miradi ya ujenzi wa visima, majosho na mabirika ya kunyweshea mifugo katika maeneo kame na yaliyoathiriwa zaidi katika wilaya za Simanjiro, Kishapu, Mpwapwa na visiwani Zanzibar.

Alisema ili kufanikisha mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, Tanzania iliandaa Mkakati wa Mabadiliko ya Tabianchi na Mpango wake wa kuchangia katika jitihada za kukabiliana na kuhimili mabadiliko ya tabianchi (Nationally Determined Contributions NDCs).

Awali, akizungumza na Mkurugenzi wa UNCDF, Waziri Jafo aliwashukuru kwa kuipatia Tanzania jumla ya Dola za Marekani 181,000 kutekeleza miradi ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi katika wilaya za Kondoa, Chamwino na Mpwapwa (mkoani Dodoma) na pia Dola za Marekani 40,000 kwa Ofisi ya Makamu wa Rais kwa ajili ya kutekeleza miradi ya NDCs.

Settings