Tanzania kuendesha mkutano mkubwa ndani ya COP 28

Nov, 11 2023

Mkutano huo utaongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan utakuwa ni fursa ya kujitangaza kimataifa kupitia Mkutano wa 28 (COP 28) wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, utakaofanyika Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu kuanzia Novemba 28 hadi 12 Disemba 2023.

Hayo yamesemwa leo Novemba 11, 2023 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo wakati akitoa tamko kuhusu ushiriki na msimamo wa Tanzania kwenye majadiliano ya mkutano huo.

Amewakaribisha wadau mbalimbali waliopo nchini kutumia fursa ya Mkutano wa COP28 kwa kuhakikisha nchi inaendelea kujitangaza na kuleta manufaa ya kijamii na kiuchumi kwa maendeleo ya wananchi wetu.

“Mkutano huu unalenga kuongeza chachu ya uwekezaji wa kimataifa kwa kutumia fursa katika sekta kwa kuvutia wawekezaji kutoka maeneo mbalimbali duniani kote ili kufahamu fursa za uwekezaji zilizopo Tanzania,” amesema.

Ameongeza kuwa mkutano huu unafanyika kila mwaka kwa mzunguko wa mabara yote matano ambapo kwa 2022, ulifanyika Sharm el Sheikh, Misri na kuleta manufaa makubwa kwa Tanzania yakiwemo upatikanaji wa miradi ya nishati jadidifu ambayo itafadhiliwa na Benki ya Dunia kwa Dola za Marekani bilioni 18.

Pia, Norway kusaidia Tanzania kuandaa Mkakati wa upunguzaji gesi joto, Shirika la Uhifadhi la Kimataifa (TNC) limefadhili tathmini ya awali kwa ajili ya kuandaa Mpango wa Matumizi ya Bahari na Tanzania imejiunga na taasisi mbalimbali zinazoshughulikia na masuala ya mabadiliko ya tabianchi.

Mkutano wa COP28 unatarajiwa kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 80,000 wakiwemo viongozi mbalimbali duniani na wadau kutoka mataifa mbalimbali ambapo kaulimbiu ya taifa ni ‘Kuimarisha Kilimo Himilivu na Uchumi wa Bluu katika Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi’



Settings