Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema Serikali ya Tanzania inathamini mchango wa wadau katika kuleta maendeleo ya nchi.
Ametoa kauli hiyo wakati akipokea gari kwa ajili ya shughuli za Ofisi ya Makamu wa Rais kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) leo Machi 19, 2024 katika Mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma,
Akimshukuru Mwakilishi Mkazi wa WFP Bi. Sarah Gordon-Gibson, Dkt. Jafo amesema Serikali inafarijika kufanya kazi na wadau mbalimbali wa maendeleo ambao wamekuwa msaada mkubwa kwa shughuli za Serikali.
Amesema kuwa gari lililotolewa na shirika hilo litasaidia katika shughuli za Ofisi hususan katika kuwahudumia wataalamu katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku ikiwemo kutembelea na kukagua miradi ya mazingira inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Pamoja na hayo, Waziri Dkt. Jafo ametoa wito kwa wadau wengine wa maendeleo kuzisaidia taasisi zingine za Serikali kwa kuzipatia vitendea ili ziweze kutekeleza majukumu yao.
“Nipende kuwashukuru WFP kwa kufanya kazi pamoja na sisi (Ofisi ya Makamu wa Rais) na Serikali kwa ujumla na niwaombe tuendeleze ushirikiano wetu kwa mustakabali wa taifa,“ amesisitiza.
Kwa upande wake Bi. Sarah amesema kuwa makabidhiano hayo ya gari ni kusherehekea ushirikiano baina ya shirika hilo na Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais.
Amesema kuwa anafarijika pia kushiriki katika hafla hiyo ya makabidhiano ya gari hilo na kuongeza kuwa litaisaidia watendaji wa Ofisi kuweza kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Bi. Sarah amemshukuru Waziri Jafo na watendaji wa Ofisi yake kwa kudumisha ushirikiano na Shirika la WFP katika shughuli mbalimbali za maendeleo zikiwemo za hifadhi ya mazingira.