Dkt. Jafo: Tanzania imeongeza wigo wa kuhifadhi ikolojia

Feb, 29 2024

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema Tanzania imeongeza wigo wa kuhifadhi ikolojia kukabiliana na uharibifu wa ardhi.

Amesema hayo wakati akishiriki Jukwaa la Utafiti wa Afya ya Udongo lililofanyika pembezoni mwa Mkutano wa Sita wa Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEA 6) unaofanyika katika Makao Makuu ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) jijini Nairobi nchini Kenya, Februari 28, 2024.

Akichangia mada katika Jukwaa hilo, Dkt. Jafo amelezea nia ya Tanzania ya kuboresha uwezo wa tafiti katika udongo pamoja na uhifadhi wa ikolojia ili kuondosha uharibifu wa ardhi unaopunguza uwezo wa uzalishaji wa chakula na uchumi kwa ujumla.

Akieleza jitihada ambazo Tanzania inazichukua katika kukabiliana na changamoto za ubora wa ardhi, amesema Tanzania imeongeza wigo wa kibajeti katika sekta ya kilimo ikiwemo kuwekeza katika kilimo cha kisasa.

Kutokana na jithada hizo, Dkt. Jafo amezitaka taasisi pamoja na kampuni za biashara kuanza kuinua fursa za kuwekeza katika tafiti za udongo ambazo ndio chachu ya uzalishaji wa malighafi na mazao ya chakula yenye ubora.

Tanzania ni miongoni mwa nchi 193 za Umoja wa Mataifa zinazoshiriki Mkutano wa UNEA 6 unaojadili masuala mbalimbali ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa bioanuai na uchafuzi wa mazingira.

Kaulimbiu ya mkutano huo kwa mwaka 2024 ni 'Juhudi Madhubuti, Jumuishi na Endelevu za Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi, Uharibifu wa Bioanuai na Uchafuzi‘.

Waziri Dkt. Jafo ameongoza Ujumbe wa Tanzania uliowajumuisha Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Abdallah Hassan Mitawi pamoja na wataalamu kutoka Ofisi hiyo.

Itakumbukwa kuwa Mkutano wa UNEA 6 ulifunguliwa Februari 26, 2024 na unatarajiwa kuhitimishwa ifikapo Machi 01, 2024.

Settings