Dkt. Jafo: Kila mtu ana wajibu wa kupanda miti

Mar, 15 2024

Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema kila mtu ana wajibu wa kupanda miti ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayoikabili dunia.

Amesema hayo wakati akishiriki zoezi la upandaji wa miti 500 katika eneo la Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Dar es salaam iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo mkoani Dar es Salaam.

Dkt. Jafo amesema kutokana na changamoto ya uharibifu wa mazingira Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais ilizindua Kampeni ya ‘Soma na Mti‘ ambayo hushirikisha wanafunzi wote nchini ili iwe endelevu katika vizazi vijavyo.

Amebainisha kuwa uharibifu wa mazingira umesababisha changamoto ya uchumi, kuwepo kwa uhaba wa umeme kutokana na ukosefu wa mvua za kutosha kwa ajili ya uzalishaji wa umeme, jambo ambalo limeibua upungufu wa uzalishaji nishati hiyo.

"Tumeshuhudia dunia nzima joto linaongezeka ambapo joto hili linasababisha athari kubwa katika maisha ya wanadamu na viumbe mbalimbali lakini sehemu nyingine ukame umeshamiri,mvua ambazo hazina utaratibu zinasababisha mafuriko", amesema Dkt. Jafo.

Aidha, ameushukuru Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa juhudi zao za kuzalisha miche ya miti kwa ajili ya kupanda nchini ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yamepelekea kupungua kwa mvua na kuongezeka kwa kina cha bahari.

Waziri Dkt. Jafo ameongeza kuwa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi imeelekeza kila halmashauri kupanda miti milioni 1.5 kwa mwaka kwa lengo la kupanda miti zaidi ya milioni 200 katika halmashauri zote ambapo katika taasisi za serikali wanafunzi kushiriki kufanya zoezi hilo.

Settings