Dkt. Jafo akutana na Mkurugenzi Mkuu NEMC

Jan, 24 2024

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Immaculate Semesi ofisini kwa Waziri jijini Dodoma.

Katika mazungumzo hayo Mhe. Dkt. Jafo amempongeza kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo ambapo amemuahidi ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake.

Pia, amesema ufanisi wa Baraza hilo katika kazi ni matokeo ya ushirikiano kati ya wafanyakazi na kiongozi wao hivyo ametoa wito kudumisha ushirikiano baina yao ili kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.

Dkt. Jafo amesema kuwa Serikali siku zote inahamasisha uwekezaji hapa nchini kutoka kwa wawekezaji mbalimbali hivyo mkurugenzi mkuu ana wajibu wa kusimamia suala hilo.

Amelitaka Baraza hilo kufanyia kazi changamoto zinazojitokeza katika sekta ya uwekezaji nchini kwa kutumia busara katika kuzishughulikia ili miradi inayoanzishwa iweze kutekelezwa pasipo kuathiri mazingira.

“Tunatambua kuwa moja ya majukumu yenu (NEMC) ni ukaguzi wa mazingira kwa kufanya uhakiki katika miradi mbalimbali ikiwemo mikubwa, ya kati na midogo lakini mna jukumu la kuwaelimisha wawekezaji ili wafuate sheria wakati huo mkizingatia kuwa hatuko kwa ajili ya kukwamisha mitradi badli kuiwezesha ifanyike na hivyo kuunga mkono juhudi za Serikali za kukuza uchumi,“ amesema.

Aidha, Waziri Dkt. Jafo pamoja na kuwapongeza na kuwatia moyo watendaji wa Baraza hilo pia amewataka kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi ili waendelee kunufaika nazo.

Kwa upande wake Dkt. Semesi ambaye aliambatana na wakurugenzi wa kurugenzi na vitengo kutoka NEMC amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa imani yake kwake.

Amemuahidi Waziri Dkt. Jafo, Ofisi ya Makamu wa Rais na Serikali kwa ujumla kuchapa kazi kwa bidii ili kufikia malengo ya kutoa huduma bora kwa wananchi kuhakikisha hifadhi endelevu ya mazingira.

Itakumbukwa kuwa, Mkurugenzi Dkt. Semesi aliteuliwa hivi karibuni kushika wadhifa huo akichukua nafasi ya Dkt. Samuel Gwamaka ambaye muda wake ulikwisha.

Settings