Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewaelekeza maafisa mazingira katika Wizara, Idara, Taasisi na Wakala kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 katika maeneo yao.
Ametoa maelekezo hayo wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Siku ya Mazingira Duniani katika viwanja vya Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma leo Juni 3, 2024.
Dkt. Biteko amesema maafisa mazingira serikalini wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha utekelezaji wa sheria ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira inasimamiwa na kutekelezwa badala ya jukumu hilo kuratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais pekee.
Amewataka kutoa elimu kwa jamii kupitia njia mbalimbali ikiwemo maonesho kwani kwa kufanya hivyo kutaisaidia kubaini mbinu na mikakati mbalimbali ya kukabiliana na athari za uharibifu wa mazingira.
Ameongeza kuwa Tanzania kama zilivyo nchi nyingine duniani imeendelea kukabiliana na athari zitokanazo na uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ukame, mafuriko na magonjwa, hali ambayo kwa kiasi kikubwa inachangiwa na shughuli za binadamu zisizo endelevu.
Amesema Serikali itaendelea kuwawezesha maafisa mazingira serikalini ili kuhakikisha wanatekeleza vyema wajibu na majukumu yao ya kila siku na kushughulikia changamoto mbalimbali ikiwemo ufinyu wa bajeti hatua inayolenga kuimarisha usimamizi endelevu wa mazingira.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema katika kuelekea Siku ya Mazingira Duniani, Ofisi imeendelea kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa uhifdhi na usimamizi wa mazingira kwa kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo uzinduzi wa miradi, kuendesha makongamano na usafi wa mazingira.
Amesema kwa takribani miaka mitatu sasa, Ofisi inaratibu matukio mbalimbali yenye kuhamasisha jamii kuhusu utunzaji wa mazingira yakiwemo usafi wa mazingira, kupanda miti na kujenga hamasa kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuhifadhi na kutunza mazingira.
Aidha Waziri Jafo amesema kupitia maonesho ya mazingira, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imejipanga kuhakikisha kuwa ajenda ya mazingira inaendelea kuungwa mkono na jamii ikiwemo kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia hatua inayolenga kulinda mazingira na afya.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule amesema mkoa huo umeendelea kutekeleza vyema sheria ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira kwa kuhakikisha maeneo yote ndani ya wilaya za mkoa huo zinaendelea kutunza na kuhifadhi mazingira ikiwemo kuhamasisha jamii kupanda miti.
Amesema kupitia Kampeni ya ‘Soma na Mti’, hadi sasa karibu asilimia 70 ya shule zote za Mkoa wa Dodoma zimepandwa miti.
Kilele cha Siku ya Mazingira kinatarajiwa kufanyika jijini Dodoma Juni 5, 2024 na Mgeni Rasmi atakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango.
Kaulimbiu inasema “Urejeshwaji wa ardhi, Ustahimilivu wa Hali ya Jangwa na Ukame”