Habari
Waziri Mkuu ataka Watanzania kubadili mtazamo hifadhi ya mazingira
Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka Watanzania wabadili mtazamo kuhusu utunzaji na uhifadhi wa mazingira na kwa kila moja kuona ni suala lake badala ya kuliona ni jambo la taasisi za usimamizi wa mazingira pekee.
“Uhifadhi wa mazingira si suala la nadharia wala kaulimbiu bali ni jambo la msingi kwa uhai wa binadamu, maendeleo ya uchumi na ustawi wa Taifa. Watanzania tunapaswa tubadili mifumo ya maisha na shughuli za kiuchumi ili kulinda mazingira kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo,” amesema.
Dkt. Mwigulu amesema hayo leo (Alhamisi, Mei 28, 2026) wakati akifungua Kongamano la Kitaifa la Wadau wa Mazingira pamoja na maadhimisho ya miaka 40 ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) yaliyofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Amesema madhara ya uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi sasa yanaonekana wazi katika maeneo mbalimbali nchini na duniani na kwamba kuna ulazima wa jamii kubadili namna ya matumizi ya ardhi, uzalishaji na matumizi ya rasilimali ili kuhakikisha mazingira yanaendelea kuwa salama na endelevu.
“Uhifadhi wa mazingira si jambo la kaulimbiu. Ni jambo halisia. Ni jambo linaloishi. Uhai wetu unategemea mazingira. Mazingira yanaweza kuendelea bila binadamu, lakini binadamu hawezi kuishi bila uwepo wa mazingira,” alisema Dkt. Mwigulu.
Aidha, Waziri Mkuu alisema ongezeko la watu, shughuli za kiuchumi na matumizi holela ya ardhi vimeongeza ushindani wa matumizi ya rasilimali, hali inayohitaji matumizi ya teknolojia za kisasa na mbinu endelevu katika sekta za kilimo, ufugaji, ujenzi na uzalishaji.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu alisifu juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kusimamia ajenda ya mazingira na nishati safi ya kupikia akieleza kuwa Serikali imeendelea kuwekeza katika miradi ya umwagiliaji, nishati safi na reli ya kisasa (SGR) ambayo inalenga kupunguza athari za uharibifu wa mazingira.



