Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais ( Muungano na Mazingira) Mhe.Mha.Hamad Masauni umekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Norway Bw. Asmund Aukrust ambapo pamoja na mambo mengine, mazungumzo yao yalijikita katika mahusiano baina ya nchi hizi mbili hususan katika hifadhi ya mazingira.
Mawaziri hao walijadiliana masuala mbalimbali ya mahusiano baina ya nchi hizi mbili ambapo Norway iliahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika masuala mbalimbali ikiwemo masuala ya mabadiliko ya tabianchi hususan kuendelea kusaidia kituo cha biashara ya kaboni NCMC pamoja na kuwezesha na kujengea uwezo Ofisi ya Makamu wa Rais katika suala zima la uratibu wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi katika Sekta zingine.
Mhe. Masauni amemfahamisha Waziri mwenzake kuwa Tanzania imeweka Mazingira bora ya wawekezaji kwa ajili ya uwekezaji na Tanzania inawakaribisha wawekezaji kutoka Norway kushirikiana na Tanzania kuwekeza katika matumizi ya taka kama malighafi ya kuzalisha umeme na mbolea.
Aidha katika majadiliano hayo Norway iliomba kuungwa mkono katika nafasi ya Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la maendeleo la umoja wa mataifa UNDP ambayo Norway kupitia mkurugenzi wake wa shirika la NORAD anakusidia kugombea nafasi hiyo.