Habari
Waziri Masauni angoza Mazingira Marathon Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni ameongoza viongozi na wanamichezo mbalimbali kushiriki mbio maalumu zilizoandaliwa na Ofisi ya Makamu ‘Mazingira Marathon’.
Mazingira Marathoni imefanyika leo Juni 5, 2026 jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani (WED) ambapo kitaifa yanafanyika Dodoma katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Center ambapo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi anatarajia kuwa mgeni rasmi.
Mhe. Masauni aliambatana na Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Reuben Kwagilwa, Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi pamoja na Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Balozi Baraka Luvanda.
Pia katika mbio hizo mwanariadha maarufu nchini, Alphonce Simbu aliweza kushiriki huku akieleza kuwa jambo hilo ni kubwa na la kupongezwa kwa kuwa unapozungumzia mazingira lazima uguse afya ya binadamu.
“Unapowashirikisha wananchi kwenye mashindano mbalimbali kama haya inaonekana namna gani afya na mazingira ni vitu ambavyo huwezi kuvitenganisha kwa kuwa uhai wetu na mazingira ni vitu muhimu na vinakwenda pamoja,” amesema Simbu.



