Waziri Jafo aipa kongole Bodi ya NEMC kwa usimamizi mzuri wa Baraza

Nov, 01 2023

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo ameipongeza Bodi ya Wakurugenzi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa utekelezaji wa majukumu yake.

Ametoa pongezi wakati akizungumza kwenye kikao cha 16 cha Bodi hiyo pamoja na Menejimenti ya NEMC kilichofanyika leo Novemba 1, 2023 jijini Dodoma.

Dkt. Jafo amesifu utaratibu wa kutembelea maeneo mbalimbali kukagua shughuli za kulinda mazingira hususan katika migodi iliyopo ya mkoani Geita na kwengineko.

“Niwapongeze mwenyekiti na timu yako badala ya kukaa tu ofisini na kuangalia takwimu kwenye makaratasi badala mmekuwa mkienda site hasa migodini na viwandani kuona uhalisia na kulisaidia Baraza mnalosimamia,” amesema.

Aidha, Waziri Jafo ametoa rai kwa Bodi hiyo kuendelea kuisimamia NEMC inapotekeleza Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 katika maeneo mbalimbali na kuwachukulia hatua wanaoikiuka.

Amesema kuwa ni jukumu la NEMC kuhakikisha wenye viwanda, migodi na maeneo ya starehe yanafuata sheria ili kudhibiti changamoto za uchafuzi wa mazingira zikiwemo utiririshaji wa majitaka, moshi au kelele na mitetemo.

Hali kadhalika Dkt. Jafo ametoa rai kwa wananchi kufuata sheria na kuepuka vitendo vya uharibifu wa mazingira ikiwemo ukataji miti holela na kuacha kuharibu vyanzo vya maji.

Settings