Habari
UNIDO yakabidhi vifaa vya kukabili uharibifu tabaka la ozoni
Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Balozi Baraka Luvanda amepokea mitambo mitatu ya utambuzi wa kemikali zinazotumika kwenye viyoyozi na majokofu pamoja na mitambo ya kusafisha kusafisha kemikali hizo na kuzichakata kwa ajili ya matumizi bila kutegemea kuagiza nje nchi.
Mitambo hiyo imetolewa na Shirika la Maendeleo ya Viwanda la Umoja wa Mataifa (UNIDO) kupitia kwa Mwakilishi Mkazi wa Bi. Lorence Ansermet katika Ofisi ndogo ya Makamu wa Rais jijini Dar es Salaam leo Mei 28, 2026.
Hatua hiyo ni mojawapo ya jitihada za Serikali za kulinda mazingira ambapo mitambo hiyo itatumika katika uvunaji, uchakataji na kutumia tena badala ya kuziachia kwenda kuharibu tabaka la ozoni.
Mitambo hiyo itakabidhiwa katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), Chuo cha Mafunzo ya Amali cha Mkokotoni, Zanzibar pamoja na Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Bagayamo, Pwani.
Akizungumza mara baada ya kupokea mitambo hiyo, Balozi Luvanda alisema tukio hilo linaonesha dhamira endelevu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na washirika wake katika kuimarisha elimu ya ufundi, ufundi, utunzaji wa mazingira na maendeleo endelevu ya viwanda.
Alisema vifaa vilivyokabidhiwa si mashine tu bali ni uwekezaji katika maarifa, ukuzaji ujuzi, uvumbuzi, na mustakabali wa mafundi na wataalamu wetu wachanga, hivyo alitoa wito kwa wanufaika wavitunze ili vidumu kwa muda mrefu.
Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa UNIDO Bi. Lorence alisema hatua hiyo ni matokeo ya Tanzania kujiunga na Mkataba wa Vienna wa Ulinzi wa Tabaka la Ozoni na Itifaki ya Montreal kuhusu vitu vinavyopunguza Tabaka la Ozoni tangu mwaka 1993.
Alisema mitambo hiyo itasaidia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambayo husababisha joto kali katika uso wa duniani kutokana na kuharibiwa kwa tabaka la ozoni.
Bi. Lorence aliongeza UNIDO na Ofisi ya Makamu wa Rais zitaendelea kushirikiana ili kuongeza ufanisi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuendelea kutoa mafunzo kwa mafundi mchundo wa majokofu na viyoyozi.
Akitoa maelezo ya awali Mkurugenzi Msaidizi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Thomas Chali alisema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazotekeleza mpango wa kudhibiti kemikali zinazoharibifu tabaka la ozoni aina ya hydrochlorofluorocarbons ifikapo mwaka 2030.
Bw. Chali alisema kuwa UNIDO imekuwa na mchango mkubwa katika utekelezaji wa mpango wa kuondosha kemikali hizo utoaji wa vifaa vya kuudumia majokofu na viyoyozi pamoja na programu za kujenga uwezo na mafunzo ya kiufundi.



