Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewasilisha mafanikio yake katika utekelezaji wa Mikataba ya Kimataifa ya Mazingira (MEAs) katika Mkutano wa Baraza la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEA-7) unaofanyika jijini Nairobi, Kenya Desemba 11, 2025.
Mafanikio hayo yamewasilishwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Festo Dugange kwenye majadiliano ya ngazi ya juu akiwasilisha uzoefu wa Tanzania katika uhuishaji na ukamilishaji wa Mkakati na Mpango wa Taifa wa Uhifadhi wa Bioanuwai (NBSAP).
Katika wasilisho hilo, Mhe. Dkt. Dugange alibainisha kuwa Serikali imekamilisha uandaaji wa Mkakati huo uliohuishwa, ukiainisha mwelekeo wa kitaifa katika kutekeleza malengo ya kimataifa ya uhifadhi wa bioanuwai.
Naibu Waziri Dkt. Dugange alisema kuwa mafanikio ya mchakato huo yametokana na mbinu shirikishi kupitia uratibu wa pamoja uliohusisha wizara mbalimbali.
“Uratibu huu umewezesha malengo ya bioanuwai kuingizwa kikamilifu katika mifumo yetu ya mipango ya maendeleo, sera za kisekta na mipango ya taasisi, hivyo kuongeza ulinganifu kati ya vipaumbele vya kitaifa na wajibu wa nchi katika mikataba ya kimataifa ya mazingira,” alisema.
Akifafanua zaidi, alisema mchakato wa NBSAP umeendeshwa pia kwa ujumuishi wa jamii, kwa kuwashirikisha wadau kutoka asasi za kiraia, taasisi za elimu ya juu, sekta binafsi na wadau wa maendeleo.
Mhe. Dkt. Dugange alisema Tanzania itaendelea kushirikiana kwa karibu na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), Sekretarieti za Mikataba ya kimataifa ya Mazingira pamoja na nchi wanachama, katika jitihada za pamoja za kufikia malengo ya KM-GBF na mikataba mingine ya kimataifa ya mazingira.
“Tanzania ipo tayari kuendelea kubadilishana uzoefu, kuimarisha ushirikiano na kuchangia utekelezaji wa malengo ya kimataifa ya mazingira,” alisistiza Mhe. Dkt. Dugange.
Katika hatua hatua nyingine, Mhe. Dkt. Dugange ameshiriki mkutano wa majadiliano pembezoni mwa Mkutano wa UNEA-7 kuhusu uwezeshwaji wa nchi uwezo wa kuandaa na upembuzi wa taarifa za kisayansi wa hali ya mazingira.
Akizungumza na Mwenyekiti wa Jopo la Serikali Mbalimbali kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (IPCC) Sir Jim Skea, Naibu Waziri alisema Tanzania iko tayari kushirikiana na taasisi hiyo katika kufanikisha masuala ya hifadhi ya mazingira.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa IPCC, Sir Skea alisema kuwa taasisi hiyo iko tayari kuwajengea uwezo wataalamu kutoka Tanzania kupitia ufadhili wa masomo ambao utaleta manufaa kwa nchi.
Majadiliano hayo yamehudhuriwa pia na Mwenyekiti wa Kundi la Majadiliano la Afrika (AGN) Dkt. Richard Muyungi ambaye pia ni Mjumbe Maalum na Mshauri wa Rais katika Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi, Mkurugenzi wa Mazingira Bi. Kemilembe Mutasa, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Mazingira Dkt. Deogratius Paul na wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais.
Mkutano UNEA-7 unawashirikisha wakuu wa nchi na serikali, mawaziri wanaoshughulikia Mazingira, wataalam na wadau wa Mazingira na maendeleo endelevu kutoka nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa, Mashirika ya Umoja wa Mataifa na asasi za kiraia.
Pia, Mkutano huo unawashirikisha wakuu wa nchi na serikali, mawaziri wanaoshughulikia Mazingira, wataalam na wadau wa Mazingira na maendeleo endelevu kutoka nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa, Mashirika ya Umoja wa Mataifa na asasi za kiraia.