Habari
Tanzania, Singapore zasaini ushirikiano biashara ya kaboni
Tanzania na Singapore zimetia saini mkataba wa makubaliano (MoU) kuhusu ushirikiano katika Biashara ya Kaboni chini ya Kifungu cha 6 cha Mkataba wa Paris katika hafla iliyofanyika Ikulu Juni 9, 2026 na kushuhudiwa na Marais wa nchi hizo.
Mkataba huo kwa Tanzania ulisainiwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni na kwa upande wa Singapore ulisainiwa na Waziri wa Nchi, Wizara ya Biashara na Viwanda, na Wizara ya Maendeleo ya Kitaifa Mhe. Alvin Tan.
Chimbuko la Maandalizi ya MoU huo ulianza, Mwezi Novemba 2025 ambapo Tanzania ilishiriki kikao cha 30 cha Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP30) kilichofanyika Belem, Brazil.
Wakati wa mkutano huo, baadhi ya wajumbe wa Tanzania walishiriki mkutano wa pembeni (Side Event) ulioandaliwa na kampuni ya S&P Global katika banda la Singapore wenye mada ya “Carbon Registry Workshop at Singapore Pavilion.
Baada ya mkutano huo, kulifanyika majadiliano ya awali na wawakilishi wa Singapore kuhusu uwezekano wa kuanzisha ushirikiano kati ya Tanzania na Singapore katika utekelezaji wa Ibara ya 6 ya Makubaliano ya Paris, hususan katika eneo la biashara ya kaboni.
Hatua hizi ziliweka msingi wa kuanzishwa kwa mchakato rasmi wa ushirikiano kati ya Tanzania na Singapore katika utekelezaji wa Ibara ya 6 ya Makubaliano ya Paris na maendeleo ya soko la kaboni.
Mwezi Januari, 2026 Afisa wa Singapore Bi. Sarah Quek kutoka Wizara ya Viwanda, Singapore aliwasiliana na Bi. Risper Koyi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais akieleza nia ya kuendelea na mazungumzo na kuomba kuunganishwa na maafisa husika wa Serikali ya Tanzania.
Bi. Koyi alishauri upande wa Singapore kuwasilisha 'Note Verbale' kupitia njia rasmi za kidiplomasia ili kuwezesha uratibu na mawasiliano ya kiufundi baada ya kupokelewa kwa Note Verbale kupitia Wizara ya Mambo ya Nje.
Mwezi Februari, 2026 Wizara ya Mambo ya Nje waliwasilisha 'Note Verbale' kutoka Singapore ikiambatanishwa na rasimu ya MoU ambapo OMR ilipitia MoU hiyo na kutoa maoni na 1 baadaye kuwasilisha rasimu Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kwa ajili ya uhakiki.
Baada ya AG kutoa maoni yake, OMR iliboresha rasimu ya MoU na kuiwasilisha Wizara ya Mambo ya Nje ambao waliwasilisha rasimu nchini Singapore kwa hatua zao.
Tarehe 25 Mei, 2026, Serikali ya Singapore iliwasilisha rasimu ya MoU baada ya kukamilisha taratibu zao za ndani ya Serikali ikiwa ni pamoja na uhakiki wa AG wao.
Baada ya hatua hiyo OMR iliwasilisha rasimu kwa AG ambapo baada ya kujiridhisha alitoa idhini kwamba MoU imezingatia maoni yake na inaweza kusainiwa. Kutokana na ushauri wa AG, OMR iliwasilisha rasimu ya MoU kwenye Wizara ya Mambo ya Nje kwa ajili ya maandalizi ya nyaraka muhimu ili MoU iweze kusainiwa tarehe 9 Juni, 2026.



