Serikali yatoa wiki tatua kuondolewa mifugo hifadhi ya Bonde la Ihefu

Sep, 26 2022

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo ametoa wiki tatu kwa wafugaji kuondoa mifugo yao katika Bonde la Hifadhi ya Ihefu wilayani mbarali mkoani Mbeya kabla ya hatua za kisheria kuchukuliwa.

Ametoa maelekezo hayo alipofanya ziara ya kikazi katika bonde hilo lililopo wilayani Mbarali mkoani Mbeya kujionea uharibifu wa mazingira wa vyanzo vya maji.

Dkt Jafo alisema wafugaji hao wamevamia bonde hilo ambalo lipo katika hifadhi ya Taifa ya Ruaha na kusababisha uharibu mkubwa wa hifadhi hiyo na vyanzo vya maji kuanza kupotea.

Aliongeza kuwa alisema mifugo hiyo imekuwa mingi kiasi kwamba imeanza kuharibu vyanzo vya maji vilivyopo katika bonde hilo la Ihefu hivyo serikali isipodhibiti basi maji yatapotea na huduma nyingine za maji nazo zitaathirika.

Waziri huyo alisema maji yanayotoka katika bonde hilo yanachangia katika Bwawa la kufua Umeme la Mwalimu Nyerere na wanyama waliopo katika hifadhi ya Taifa ya Ruaha wanategemea maji hayo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera alisema ng’ombe ni wengi kuliko wanyama katika hifadhi hiyo kwenye Bonde la Ihefu na hivyo wanaharibu vyanzo vya maji.

Alisema operesheni ya kukamata mifugo inaendelea huku akimshukuru Waziri Jafo kwa kufika katika eneo hilo na kutoa maelekezo ambayo yatasaidia katika kutatua changamoto hiyo.

Settings