Habari
Mhandisi Masauni: Serikali imeimarisha ushirikiano kulinda mazingira
Serikali ya Awamu ya Sita pamoja na mambo mengine imeimarisha zaidi ushirikiano wa kimataifa na kutoa mchango mkubwa katika masuala ya kikanda na kimataifa yanayohusu mazingira na mabadiliko ya Tabianchi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni ameyasema hayo wakati akiongea na Waandishi wa Habari Unguja, Zanzibar Machi 3, 2026 wakati akitoa kauli ya Serikali katika Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Afrika inayoadhimishwa kila mwaka Machi 3.
Amesema kupitia ushawishi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika medani ya kimataifa, Tanzania imepata fursa za kuongoza masuala mbalimbali ya kikanda ambayo ni pamoja na kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika - Misheni 300 uliofanyika Januari 27 hadi 28 Januari, 2025 jijini Dar es Salaam.
Pia Tanzania ilifanikiwa kuwa mjumbe wa kudumu wa Kamati ya Umoja wa Afrika ya Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Mhandisi Hamad Masauni kuwa Makamu Mwenyekiti wa Mkutano wa Nane wa Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEA - 8) kuanzia Desemba 2025 hadi Desemba 2027.
Amesema Maendeleo na ukuaji wa taifa lolote duniani pamoja na ustawi wa watu wake vimefungamana na hali na ubora wa mazingira. Hali ya mazingira ikiwa imara ukuaji wa uchumi na ustawi wa watu pia huwa imara.
“Tarehe 3 Machi ya Kila mwaka, Bara la Afrika huadhimisha Siku ya Mazingira Afrika, siku hii adhimu iliasisiwa mwaka 2002 na Baraza la Mawaziri la Umoja wa Afrika ikiwa ni moja ya maazimio muhimu ya Umoja wa Afrika katika kuhimiza nchi wanachama na Bara la Afrika kutunza na kuhifadhi mazingira,
“Kauli mbiu ya siku hii kwa mwaka huu ni ‘Assuring Sustainable Water Availability and Safe Sanitation Systems to Achieve the Goals of Agenda 2063". Ambayo tafsiri yake ni: "Uhakika wa upatikanaji Endelevu wa Maji na Mifumo Salama ya Usafi wa mazingira ili kufikia Malengo ya Ajenda 2063,” amesema Mhe. Masauni.
Amesema, kauli mbiu ya siku ya Mazingira kwa Afrika mwaka huu inahusu Uhakika wa upatikanaji Endelevu wa Maji na Mifumo Salama ya Usafi wa mazingira kwa maendeleo endelevu inatukumbusha umuhimu wa kutekeleza mipango shirikishi ambapo mtu na taasisi ni muhimu kushiriki ipasavyo kwa faida ya nchi.
“Kwa kutambua uhalisia huu, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imedhamiria kufungamanisha kwa vitendo masuala ya mazingira, mabadiliko ya tabianchi na maendeleo endelevu”.
Ameongeza kuwa Dira 2050 imeweka nguzo adhimu inayohusu Uhifadhi wa Mazingira na ustahimilivu dhidi ya Mabadiliko ya Tabianchi. Vile vile, Ilani ya CCM imeweka masuala ya mazingira na mabadiliko ya Tabianchi kama mojawapo ya masuala muhimu yatakayozingatiwa katika kipindi cha mwaka 2025 – 2030.
Mhe. Masauni amesema Dunia inapitia katika changamoto kuu tatu za Mazingira ambazo ni: Upotevu wa Bioanuai; uchafuzi wa Mazingira kutokana na vyanzo mbalimbali pamoja na Mabadiliko ya Tabianchi.
Amesema, uhalisia huu unakumbusha umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kuimarisha uhifadhi wa mazingira pamoja na ufumbuzi wa pamoja wa changamoto za mazingira, ni kwa muktadha huu, Tanzania ni nchi mwanachama wa mikataba mbalimbali inayohusu hifadhi na usimamizi wa mazingira.



