Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Prof. Peter Msoffe amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Kitengo cha Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP) Bi. Mirey Atallah.
Mazungumzo hayo yamefanyika pembezoni mwa Mkutano wa 30 wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP3) uliofanyika katika Jiji la Belém, Brazil.
Prof. Msoffe amemueleza Mkurugenzi huyo kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana na UNEP katika maeneo mbalimbali ikiwemo kuimarisha mifumo ikolojia ili kuleta uwiano wa viumbe hai na mazingira.
Alisema Tanzania imejaliwa kuwa na vyanzo vingi vya maji vikiwemo mito, maziwa na bahari ambavyo ni muhimu katika uhai wa mwanadamu na kwa hiyo Serikali inaishirikisha jamii katika kuvitunza.
Naibu Katibu Mkuu alieleza kuwa kutokana na uwepo wa vyanzo hivyo vya maji, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kuratibu Sekta ya Uchumi wa Buluu ambao tayari Sera yake ilishazinduliwa na
Akiendelea na mazungumzo hayo, Prof. Msoffe alimueleza mkurugenzi huyo kuwa urejelezaji wa plastiki na malighafi zingine ni shughuli muhimu nchini Tanzania kwani inasaidia katika kutunza mazingira na kuzalisha bidhaa mbalimbali na hivyo kusaidia kukuza uchumi.
“Tunawaomba UNEP muendelee kushirikiana pamoja na Serikali yetu katika kusaidia kuhakikisha tunakabiliana na kuziondosha kabisa taka za plastiki kwa kuwa na mifumo thabiti ya urejelezaji,” alisema Prof. Msoffe.
Kwa upande wake Bi. Mirey aliishukuru Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa ushirikiano wake na shirika hilo hususan katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya hifadhi ya mazingira.
Alitolea mfano Mradi wa Kujenga Uwezo wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi katika Mazingira ya Mkoa wa Kigoma unaofadhiliwa na UNEP kupitia Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi (GCF) unaoratibiwa chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC).
Bi. Mirey alisema kuwa shirika hilo litaendelea kufadhili mradi huo kupitia ambao unaoelenga kuzisaidia jamii zinazozunguka kambi za wakimbizi katika kuhakikisha misitu inarejea.
Pia, alizungumzia mradi wa Bonde la Ziwa Victoria unaolenga kusaidia jamii inayozunguka wenye thamani ya dola milioni 100 sanjari na kuunga mkono miradi ya upandaji wa mikoko kwenye pwani ya Dar es Salaam.
Katika mkutano huo Prof. Msoffe aliambatana na Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Kemilembe Mutasa na wataalamu mbalimbali kutoka Ofisi hiyo na taasisi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.