​Ofisi ya Makamu wa Rais yatoa mafunzo ya kurejeleza gesi

Jan, 27 2020

Matokeo ya kuharibika kwa Tabaka la Ozoni ni kuruhusu mionzi zaidi ya urujuani (UV-B) kufikia uso wa ardhi hivyo kutishia afya ya viumbe hai katika ikolojia mbalimbali. Tafiti zimethibitisha kuwa kumong’onyoka kwa tabaka la ozoni kumetokana na kurundikana angani kwa kemikali/gesi zinazotumika kwenye mafriji, viyoyozi na mitambo ya kupoozea joto.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Faraja Ngerageza jijini Dar es Salaama wakati akifungua warsha ya mafunzo ya kurejeleza gesi zilizotumika na madhara yatokanayo na matumizi ya gesi feki iliyotolewa kwa Wakufunzi wa Chuo cha VETA.

Alisema kuwa Serikali imeaandaa Programu mbali mbali kwa ajili ya utekelezaji wa Itifaki ya Montreal. Mkakati wa kitaifa chini ya mipango ya nchi ni pamoja na kuimarisha uwezo wa Taasisi zinazohusika na utekelezaji wa Itifaki ya Montreal, kukusanya takwimu za uingizaji na matumizi ya kemikali zinazoharibu tabaka la ozone.

Pia uhamasishaji juu ya umuhimu wa kulinda tabaka la ozoni, kujenga uelewa kwa Wakufunzi juu ya urejelezaji wa gesi iliyokwisha tumika katika mafriji, viyoyozi na mitambo ya kupozea joto, Kuhamasisha matumizi ya kemikali rafiki kwa tabaka la ozoni na Kuweka utaratibu wa udhibiti wa uingizaji na matumizi ya kemikali zinazoharibu tabaka la ozoni.

Ofisi ya Makamu wa Rais imekuwa na utaratibu wa mara kwa mara kuandaa warsha za mafuzo ya aina hiyo kwa Wakufunzi wa vyuo vya VETA Nchini wanaohusika na masuala ya mafriji, viyoyozi na mitambo ya kupoozea joto. Washiriki wa warsha hiyo wametoka katika vyuo vya VETA vifuatavyo Dar es Salaam, Zanzibar, Kilimanjaro, Arusha, Mbeya, Mwanza, Morogoro, Pwani na Kigoma.

Settings