Ofisi ya Makamu wa Rais yaelezea mikakati ya kuhifadhi mazingira

Oct, 25 2023

Kutokana na maandalizi ya Taarifa za Hali ya Mazingira nchini, Serikali na wadau wameweza kubuni na kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuhifadhi mazingira nchini.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis wakati akiwasilisha Taarifa ya Hali ya Ufanisi katika Uchakataji na Uandaaji wa Taarifa za Hali ya Mazingira kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge jijini Dodoma leo Oktoba 24, 2023.

Amesema miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na Taarifa ya pili na ya tatu ya hali ya mazingira nchini kuainisha uwepo wa mikakati na mipango mingi ya kisekta na matambuka katika hifadhi na usimamizi wa mazingira.

”Ili kurahisisha uratibu na kuleta ufanisi katika utekelezaji wa mipango na mikakati hiyo umeandaliwa Mpango Kabambe wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, 2022-2032, unaoanisha vipaumbele vya kitaifa katika kutekeleza mipango na mikakati hiyo kwa miaka kumi. Katika maeneo ya kipaumbele mpango huo unaonesha changamoto, visababishi vya changamoto hiyo, hatua zilizokwisha chukuliwa, maeneo mahsusi ya vipumbele na hatua za kuchukua,” amefafanua Mhe. Khamis.

Akiendelea kuwasilisha taarifa hiyo, amesema katika udhibiti wa uchafuzi wa mazingira mafanikio yaliyopatikana kutokana na mapendekezo ya taarifa hizi ni pamoja na kupiga marufuku matumizi ya vibebeo vya plastiki ambapo takriban viwanda 70 vimeanza kutumia teknolojia rafiki kwa mazingira.

Hali kadhalika, kuhifadhiwa kwa asilimia 40 ya eneo lote la nchi kwa ajili ya makazi ya viumbe pori na bioanuai ambapo hadi kufikia mwaka 2018, jumla ya misitu ya hifadhi asili 12 yenye ukubwa wa hekta 305,000 imehifadhiwa.

Naibu Waziri Khamis amefafanua kuwa Taarifa ya pili na ya tatu ziliainisha uharibifu wa misitu utokanao na ukataji miti kwa ajili ya kuni na mkaa na kufungua mashamba mapya.

”Katika kukabiliana na changamoto ya ukataji miti tumeanzisha kampeni ya upandaji miti, ambapo kila halmashauri imeendelea kutakiwa kupanda miti milioni 1.5 kwa mwaka kulingana na msimu wa mvua katika eneo husika. Pia, ili kujenga msingi wa vijana wetu imeanzishwa kampeni ya Soma na Mti ambapo kila mwanafunzi anahamasishwa kupanda mti na kuutunza awapo shuleni,” amesema Mhe. Khamis.

Wakichangia taarifa hiyo baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira waimeipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kuratibu na kusimamia vyema kampeni za upandaji miti ikiwemo ya Soma na Mti pamoja na Mpango Kabambe wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira.

Wameshauri kuwa wanafunzi wajengewe uelewa kuhusu ni aina gani za miti inayopaswa kupandwa katika maeneo ya shule zao zoezi hilo liwe na tija.

Settings